WAAJIRI sekta binafsi Mkoa wa Dodoma, wametakiwa kufuata Sheria na taratibu za uajiri ikiwa ni pamoja na kulinda haki za wafanyakazi wao kwa kuhakikisha wanatoa Mikataba ya kazi kwa wafanyakazi wao ili waweze kupata stahiki zao muhimu pindi muda wa ajira unapokwisha.
Hayo yamebainishwa leo Mei Mosi, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary S. Senyamule kwenye hotuba yake kwa wafanyakazi wa Taasisi za umma na binafsi waliojitokeza kushiriki Maadhimisho ya Sherehe za wafanyakazi (Mei Mosi) Kimkoa kwenye uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
“Serikali ina thamini mchango wa wafanyakazi ndio maana tunaadhimisha siku hii. Nitoe wito kwa waajiri sekta binafsi kuhakikisha wanatoa mikataba ya ajira kwa wafanyakazi wao na pia kuhakikisha wanapeleka mafao yao kwenye mifuko ya hifadhi za jamii.
“Waajiri ambao watakiuka hili, nitoe shime kwa mifuko hiyo kufuata taratibu za kisheria dhidi ya waajiri wasiowasilisha mafao hayo. Pia , niwasisitize Watumishi wachache wasiotimiza wajibu wao, timizeni wajibu kwa Sheria na taratibu za utumishi “ Amesema Mhe. Senyamule.
Kadhalika, Mratibu wa vyama vya wafanyakazi Mkoa wa Dodoma Bw. Sylvester Mshanga akisoma risala ya wafanyakazi mbele ya mgeni rasmi, amemshukuru Mhe. Rais kwa kujali vilio vya wafanyakazi kwani katika kipindi cha miaka mitatu amepandisha madaraja kwa Watumishi, ameondoa tozo ya 6% kwa mikopo ya Elimu ya juu, kulipa Watumishi walioondolewa kazini kutokana na changamoto ya vyeti n.k.
Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani maarufu kama Mei Mosi hufanyika kila mwaka nchini na mwaka huu, Kitaifa yamefanyika kwenye Mkoa wa Arusha huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa ndiye mgeni rasmi. Maadhimisho hayo yameongozwa na kauli mbiu isemayo “Nyongeza ya Mishahara ni Msingi wa Mafao Bora na Kinga dhidi ya hali ngumu ya maisha”
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.