Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WAANDISHI wa habari wameshauriwa kujitokeza kuhesabiwa na kuhamasisha makundi mengine katika Sensa ya watu na makazi itakayofanyika tarehe 23 Agosti, 2022 nchini.
Rai hiyo ilitolewa na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe wakati wa majumuisho ya ziara ya kutembelea mabanda ya maonesho ya Nanenane iliyoongozwa na mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Dkt. Khamis Mkanachi kwenye banda la Nanenane kanda ya kati katika viwanja vya Nzuguni jijini hapa.
Prof. Mwamfupe alisema kuwa yupo tayari kuhesabiwa. “Mimi nipo tayari kuhesabiwa ili kuweka mipango bora ya maendeleo kwa wananchi wetu, bila shaka nanyi waandishi wa habari mpo tayari kuhesabiwa” alisema Prof. Mwamfupe.
Alisema kuwa Sensa hiyo ni muhimu na itaisaidia serikali kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo. “Ukishafahamu uhitaji na ukiwa na takwimu sahihi ni rahisi kupeleka miradi ya maendeleo. Waandishi wa Habari mtusaidie pia kuihamasisha na kuielimisha jamii juu ya umuhimu wa Sensa kwa nchi yetu” alisema Prof. Mwamfupe.
Kwa upande wake Afisa habari katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Theresia Nkwanga alisema kuwa waandishi wa habari wanawajibu wa kuhamasisha na kuelimisha juu ya umuhimu wa Sensa ya watu na makazi. “Waandishi wa habari wanawajibu wa kuhamasisha jamii ili ijitokeze kuhesabiwa. Sensa itaisadia serikali kupanga mipango ya maendeleo ambayo italinufaisha taifa kwa ujumla wake kupitia huduma za kijamii zitakazotolewa” alisema Theresia.
Maonesho ya shughuli za kilimo na mifugo mwaka 2022 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Agenda 10/30: kilimo ni biashara, shiriki kuhesabiwa kwa mipango bora ya kilimo, mifugo na uvuvi”.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.