“ASANTENI sana kwa kuja majirani zetu, japo mara nyingi huwa hatutembeleani hadi tukutane kwenye vikao… nimefurahi sana kuwaona, karibuni na tutaendelea kutembeleana kama ndugu” alisema Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Profesa Davis Mwamfupe alipokuwa akiwakaribisha wabunge kutoka nchi ya Kenya waliokuja kwenye ziara ya kujifunza jinsi ya kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati Jijini Dodoma.
Wabunge hao wamefanya ziara ya siku mbili kutembelea miradi ya Jiji la Dodoma na kujifunza ni jinsi Mfuko wa Maendeleo wa Jimbo unavyofanya kazi jijini Dodoma ili kutekeleza malengo yake kwa wananchi.
Moja ya wabunge hao anayetokea jimbo la Turbo na Embakasi Central Janeth Sitienei alisema "sisi kama wabunge wa Kenya tunamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anazozifanya ikiwemo kusimamia fedha vizuri katika miradi ambayo inailetea nchi faida".
Mbunge mwingine Elgon Fred Kapondi alisifia miradi mikubwa inayotekelezwa na Halmashauri ya Jiji kama vile miundombinu ya barabara, uwanja wa ndege, soko kuu, kituo cha mabasi na eneo la kupumzikia, "...kwa kweli mnaitaji pongezi" alisisitiza Kapondi.
Awali wabunge hao walifanya mazungumzo na Mstahiki Meya pamoja na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi kabla ya kupitishwa katika miradi kadhaa mikubwa inayotekelezwa na Halmashauri ikiwemo kituo kituo kikuu mabasi, soko kuu na eneo la mapumziko na michezo mbalimbali (Chinangali Recreational Park) lililopo jirani na uwanja wa Ndege wa sasa hapa Jijini.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.