WABUNGE wamepongeza kupelekwa Bungeni Muswada wa Sheria wa Serikali Mtandao, utakaoweka mfumo thabiti wa kisheria utakaozuia urudufu wa mifumo na miundombinu ya serikali mtandaoni.
Muswada huo pia utabadili Wakala ya Serikali Mtandao kuwa mamlaka, itakayokuwa na jukumu ya usimamizi uratibu na udhibiti, urekebu na utekelezaji wa serikali mitandaoni.
Wakichangia muswada huo baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Uwekezaji, Angella Kairuki kuwasilisha bungeni kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, George Mkuchika bila kujali tofauti za vyama vyao, walisema muswada huo umekuja wakati wake.
Akichangia Mbunge wa Busokelo, Fred Mwakibete (CCM) alisema muswada huo ni muhimu kwa Tanzania kuingia katika mitandao na kuendana na maendeleo ya duniani katika mawasiliano mbalimbali.
“Ni wakati sahihi kwa serikali kuleta mtandao huo ili tuanze kutumia IT na ICT kufanyia kazi kwani sasa dunia ipo kwenye kiganja, hivyo biashara, viwanda, utafiti, kilimo, maji, fedha na zinafanyika kupitia mitandao,” alisema Mwakibete.
Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema) alisema muswada huo ni muhimu, hata kama umekuja bila kujiandaa vya kutosha, kwani elimu itolewe kwanza kwa wananchi na kujenga mazingira ya wananchi kuwa na simu za mikononi.
Mbunge wa Welezo, Saada Mkuya (CCM) alisema serikali inatakiwa kuwa makini na watu wasiopenda maendeleo ya serikali mtandao, ambao wataingiza mitandao feki kama vifaa vya umeme vilivyo feki.
Alisema baadhi ya taasisi zilianza siku nyingi ikiwemo Hazina na NHC, hivyo kuwa na sheria hiyo kutasaidia kufanyika kwa ubora zaidi na kupanua huduma kwa jamii.
Awali, akisoma maelezo, Kairuki alisema ni muswada muhimu katika kurahisisha matumizi ya serikali mtandao na kuongeza ufanisi na ubora wa huduma zinazodhibitwa na Wakala wa Serikali Mtandao.
“Muswada huo unakusudia kutunga kwa Sheria ya Serikali Mtandao ya Mwaka 2019 itakayoanzisha Mamlaka ya Serikali ya Mtandao itakayokuwa na jukumu la kusimamia na kudhibiti shughuli za serikali mtandao nchini,” alisema. Kairuki alisema Serikali Mtandao nchini itaimarisha ukusanyaji mapato ya serikali, kuimairisha usimamizi wa matumizi ya rasilimali za TEHAMA katika taasisi za umma.
“Utaboresha mazingira ya biashara (leseni, kodi, benki, usimamizi wa ardhi, utoaji wa hati za kusafiria) na kuimairisha utendaji kazi serikalini (uwazi, ufanisi, uwajibikaji, kupunguza gharama za uendeshaji, kudhibiti na kupunguza vitendo vya rushwa na utoaji wa huduma kwa umoja kupitia TEHAMA,” alisema Kairuki.
Akisoma maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Dk Jasson Rweikiza alisema suala la usalama wa Serikali Mtandao, lizingatiwe kwa kiwango cha juu na iwapo litavamiwa linaweza kukwamisha shughuli za serikali zinazotolewa kwa kutumia mitandao.
“Mtendaji Mkuu wa Mamlaka na wasaidizi wake, wawe ni watu wenye historia nzuri ya kiutendaji serikalini au katika taasisi za umma, wenye moyo wa kizalengo na wanaotanguliza maslahi ya taifa kwanza,” amesema.
Kwa kuzingatia kasi ya maendeleo ya mabadiliko ya teknolojia TEHAMA duniani, mamlaka hiyo inapaswa kuwezeshwa kifedha na kiufundi ili kuweza kwenda sambamba na kasi ya mabadiliko hayo.
Akisoma maoni ya msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Catherine Ruge kwa niaba ya Ruth Mollel (Chadema) alisema pamoja na nia nzuri ya uanzishwaji wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, kambi hiyo inashauri kwamba malengo hayo yanaweza kukwamishwa, kama serikali haitarekebisha baadhi ya sheria ambazo zinadhibiti mawasiliano mitandaoni na upatikanaji wa taarifa na takwimu mbali mbali serikalini.
Chanzo: www.habarileo.co.tz
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.