Halmashauri ya Jiji la Dodoma imefanya kikao na wadau wa elimu kwa lengo kuweka mipango ya kupandisha kiwango cha ufaulu hadi kufikia nafasi ya kwanza kitaifa na kulinda hadhi ya makao makuu ya nchi.
Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa shule ya sekondari Umonga kilihudhuriwa na wadau mbalimbali wa elimu akiwepo Mkuu wa Wilaya, kaimu Mkurugenzi wa Jiji, mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Naibu Meya wa Jiji la Dodoma, mbunge wa viti maalum, Madiwani, Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma na wadau wengine wa elimu.
Mgeni rasmi katika kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Patrobas Katambi alisema kuwa jamii ina wajibu kuhakikisha kiwango cha ufaulu kinapanda. “Ndugu wajumbe wa kikao hiki, jukumu la kuhakikisha elimu inapanda katika Jiji letu ni jukumu langu mimi, wewe, wao na wale ili shule zetu za Serikali zipande na kuwa na thamani ya kuwa nafasi ya kwanza kitaifa” alisema Katambi.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa sekta ya elimu katika Jiji la Dodoma inakabiliwa na changamoto mtambuka zinazoigusa jamii nzima. Changamoto hizo zinahusisha wanafunzi, wazazi, walimu, wadau wa elimu, serikali na nyenzo za kufundishia na kujifunzia.
Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma inafanya vizuri katika sekta elimu. “Ninaipenda sana Dodoma na ni mdau mkubwa wa elimu. Nimetoa vishikwambi 500 vyenye thamani ya shilingi bilioni 1 kwa shule za Dodoma zenye umeme zilizoko pembeni ya mji. Nimejenga shule kwa pesa zangu mwenyewe na mheshimiwa Jafo ataifungua siku sio nyingi huko Nala.
Kupitia mfuko wa Jimbo nitatoa mifuko 80 ya ‘cement’ na matofali 1,000 kwa kila Kata ili kutatua changamoto za vyumba vya madarasa na matundu ya choo. Natamani sana haya majengo ya vyuo yatumiwe na wanadodoma wenyewe maana watu wakitaka tu mdada wa kazi za ndani wanatizama Dodoma hiyo inaniumiza sana natamani hali hiyo iishe katika Jiji letu”, alisema Mavunde.
Akiwasilisha taarifa ya mwenendo wa elimu katika Jiji la Dodoma, Afisa elimu sekondari, Martin Nkwabi alisema kuwa wapo katika mapinduzi ya elimu jijini Dodoma. Katika mapinduzi hayo, shule zote za serikali na binafsi zitatumia mfumo unaofanana.
“Tutahakikisha tunazuia mimba, utoro kazini na darasani, kuziba pengo la upungufu wa walimu, vyumba vya madarasa na vyoo, maabara, maktaba, madawati na nyenzo zote za kufundishia na kujifunzia, hivi vyote vitaleta mabadiliko ya elimu Dodoma” alisema Nkwabi.
Kwa upande wake mwalimu mstaafu, Kashozi alitoa maoni kwa kusema kujali muda ni kitu cha msingi sana ambacho watu wengi hawana, kingine ni nidhamu. Huyu ni kiongozi wa kila kitu katika maisha ya kila siku ya kazi kama mwanafunzi, mwalimu, mzazi na kila mtu atakuwa na nidhamu elimu yetu itapanda kwa kiasi kikubwa na tutapata matokeo mazuri kufikia hata kuwa wa kwanza kitaifa, aliongeza Kashozi.
Nae Afisa Elimu Msingi katika Jiji hilo, Joseph Mabeyo alisema kuwa Katika matokeo ya kidato cha nne, Halmashauri ya Jiji la Dodoma imepanda kutoka nafasi ya 67 katika halmashauri zote nchini hadi kufikia nafasi ya 38 ambayo ndiyo ya mwaka 2019. Mipango ya kuifikisha Dodoma nafasi ya kwanza inaendelea, aliongeza.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu Mheshimiwa Anthony Mavunde ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini akiongea kwenye kikao cha wadau wa elimu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Martin Nkwabi (aliyesimama) akielezea mafanikio ya kielimu kwa mwaka 2019 na mikakati iliyopo ya kuboresha elimu Jijini Dodoma.
Mgeni rasmi wa kikao cha wadau wa elimu wa Jiji la Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini Mhe. Patrobas Katambi akiongea na wajumbe kuhusu nia na malengo yatakayowezesha kufikia mafanikio makubwa zaidi ya elimu wilayani Dodoma mjini.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.