WADAU wa maendeleo hasa wanaoshughulikia masuala ya wanawake wameaswa kuelekeza rasilimali na afua zaidi katika kuwasaidia wanawake wanaoishi vijijini ambao ndio wazalishaji wakubwa wa malighafi za viwanda na mazao ya chakula katika kaya na ndio wachangiaji wakuu wa pato la Taifa.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameyasema hayo alipozungumza na wananchi katika kata ya Mang'ula, Halmashauri ya mji wa Ifakara, wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro aliposhiriki maadhimisho ya siku ya kimataifa ya mwanamke anayeishi kijijini, Oktoba 15, 2022.
Waziri Dkt. Gwajima amesema kuwa Wanawake hasa wa vijijini ndio wanapata changamoto nyingi zaidi kutokana na mgawanyo wa majukumu katika familia, uwezo mdogo wa kipato, elimu na ujuzi duni, mila na desturi kandamizi, ukubwa wa wategemezi katika kaya na udhaifu wa miundombinu iliyopo vijijini, hivyo ni muhimu sana kuimarisha ustawi na maendeleo yao ili kupunguza changamoto zinazowakabili.
"Serikali imeamua kuimarisha ustawi na maendeleo ya mwanamke anayeishi kijijini ili kuleta mabadiliko endelevu yatakayonufaisha jamii kwa ujumla na kumpunguzia huyu mama anayeishi kijijini athari mbalimbali zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na njaa, ukame na mafuriko yanayoweza kuleta madhara ya kuharibu nyumba zilizo dhaifu". Amesema Dkt. Gwajima.
Aidha, ameongeza kwamba maadhimisho hayo yanatumika kuhamasisha wadau kuelekeza rasilimali kwa wanawake waishio vijijini ambapo matokeo yake yatawezesha kuainisha mbinu za kuamsha ari ya wadau kuboresha hali na mazingira ya vijijini kwa kutoa kipaumbele katika kushughulikia changamoto, mahitaji yao na kuunga mkono jitihada za wanawake waishio vijijini na kuandaa mifumo ya kukusanya takwimu za mchango wa wanawake waishio vijijini katika kuinua uchumi wa Taifa.
Vile vile, Waziri Dkt Gwajima amesema majukumu hayo yatajenga uwezo wa wanawake waishio vijijini kuthubutu kushiriki katika siasa, uongozi na nafasi za kutoa maamuzi ili waweke msukumo katika kuelekeza rasilimali, nyenzo za uzalishaji mali na huduma za kifedha kwa vikundi vya wanawake na SACCOS zilizopo vijijini
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.