NA. Dennis Gondwe, DODOMA
WILAYA ya Dodoma katika maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania wadau wa maendeleo wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kupanda miti ya aina mbalimbali kwa ajili ya kupendezesha Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alipokuwa akizindua zoezi la upandaji miti na kupendezesha Halmashauri ya Jiji la Dodoma iliyofanyika katika barabara ya Kuu katikati ya Jiji la Dodoma.
Shekimweri alisema kuwa Wilaya ya Dodoma inapoadhimisha miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania bara imepanga kupanda miti 61 ya aina mbalimbali katika vyungu vya kisasa na maridhawa kwa lengo la kupendezesha mji.
Akiongelea maendeleo ya Wilaya ya Dodoma, Shekimweri alisema kuwa Dodoma imepiga hatua kubwa ya kimaendeleo ikilinganishwa na miaka ya nyuma. “Dodoma ya leo imepiga hatua kubwa ya maendeleo. Tupo hapa kuenzi mema ya wilaya yetu kwa kutunza mazingira na kupanda miti. Nichukue fursa hii kuwaalika wadau kujitokeza kwa wingi kuunga mkono jambo hili muhimu kwa wilaya yetu” alisema Shekimweri.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Dodoma kuzindua zoezi la upandaji miti na kupendezesha Halmashauri ya Jiji la Dodoma Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alisema kuwa ratiba ya maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru ilianzia Kituo Kikuu cha Mabasi Dodoma kwa kufanya usafi wa pamoja na kupanda miti. Alisema kuwa zoezi la kupanda miti na kuipendezesha Dodoma kuna linalenga kuwapa wananchi mazingira safi, bora na yanayovutia.
Awali Mkuu wa Kitengo cha udhibiti wa taka ngumu Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro alisema kuwa zoezi hilo la upandaji miti na kupendezesha Halmashauri ya Jiji la Dodoma linatekelezwa kwa mara ya pili. Alisema kuwa awali lilitekelezwa katika karabara ya Kuu kuanzia maeneo ya Chako ni Chako hadi mzunguko wa Whimpy. “Awamu ya kwanza zoezi lilihusisha upandaji miti aina ya “golden palm” katika vyungu 30 vya kimkakati vilivyopendezesha Jiji la Dodoma na kulifanya kuwa kivutio ndani na nje ya mipaka yake” alisema Kimaro.
Maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania tarehe 8 Desemba yameadhimishwa kwa kufanya usafi na kupanda miti katika Kituo Kikuu cha Mabasi Dodoma, kupanda miti ya kupendezesha Jiji katika barabara pamoja na shughuli nyingine.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.