Na. Shaban Ally, DODOMA
WADAU wa mazingira wameshauriwa kutunza miti inayopandwa ili iweze kufikia lengo la upandwaji wake katika kuboresha mazingira wilayani Dodoma.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Jabir Shekimweri aliposhiriki zoezi la upandaji miti katika Hospitali ya Mirembe katika maadhimisho ya wiki ya mazingira kitaifa.
Shekimweri alisema kuwa wadau wa mazingira wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha miti inayopandwa inatunzwa ili iweze kustawi vizuri. Alisema kuwa miti iliyopandwa katika hospitali hiyo isaidie kuboresha mazingira ili iwe moja ya kivutuo cha utalii katika wilaya hiyo jambo litakaloipatia mapato Halmashauri ya Jiji. "Ili kuweza kumvutia mtu kuja kutalii katika eneo hili, ni lazima tupande miti itakayovutia watu kupumzika na kufanya utalii katika eneo hilo", alisema Shekimweri.
Kwa upande wake Afisa Mazingira wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) bwana Aziz alisema kuwa wakala unalipa suala la mazingira kipaumbele kwa kupeleka Nishati. "Sisi kama Wakala wa Nishati Vijijini tunashiriki kwa vitendo katika suala zima la utunzaji wa Mazingira katika maeneo yetu kwa kupeleka huduma ya Nishati katika maeneo husika" alisema Azizi.
Zoezi la upandaji miti katika maadhimisho ya wiki ya Mazingira kitaifa lilifanyika katika eneo la Hospitali ya Mirembe, Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kuratibiwa na (REA).
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.