WADAU wa Nyuki wameshauriwa kufungua duka la mazao ya Nyuki Jijini Dodoma ili kuongeza wigo wa kujitangaza na urahisi wa upatikanaji wa asali.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda alipokuwa akifunga maadhimisho ya siku ya Nyuki duniani yaliyofanyika katika Viwanja vya Nyerere Square Jijini hapa leo.
“Dodoma tulishakubaliana kufanya mkutano wa wadau wa ufugaji Nyuki, natamani Dodoma tupate eneo ambalo litakuwa ni duka la asali kwa mkoa wa Dodoma…lazima wadau wa asali tukae eneo linaloonekana ili tuuze asali” alisema.
Waziri Mkuu huyo Mstaafu alisema kuwa, kufunguliwa kwa duka la uuzaji asali kutawasaidia wauzaji walio maeneo ya pembezoni kufahamika na bidhaa zao kuuzika kwa urahisi.
Akiongelea umuhimu wa Nyuki, alisema mazao ya nyuki ni chakula, malighafi za viwandani na dawa na kwamba fursa kwa Watanzania ni kubwa kupitia ufugaji nyuki nchini.
“Tanzania ina uwezo wa kuzalisha tani 138,000 za asali na tani 9,200 za nta kwa Mwaka, lakini uzalishaji wa sasa ni tani 4,800 za asali na tani 324 za nta,hivyo fursa bado ni kubwa” alisema Pinda.
Awali, Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangala alisema kuwa utamaduni wa kufuga Nyuki umepungua sana hivyo msukumo unahitajika na kwamba Serikali imedhamiria kuanzisha chama cha ushirika cha wafugaji nyuki ambacho kitaanza na Mikoa 10 katika Mwaka huu.
Alisema kuwa, katika Mikoa hiyo, kila Wilaya itakuwa na kiwanda cha kuchakata mazao asali huku akidai kuwa changamoto kubwa inayotarajiwa ni kiwango kidogo cha asali kinachozalishwa na wadau.
Siku ya Nyuki duniani ni azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kuwa tarehe 20 Mei, kila mwaka ni siku ya Nyuki duniani kutokana na umuhimu wao katika kuhakikisha ekolojia inakuwa endelevu.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.