WADAU wa soka katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wanaimani na timu ya Tanzania (Taifa stars) kuwa itaifunga timu ya Taifa ya Kenya (Harambee stars) katika mashindano yanayoendelea ya kombe la mataifa ya Afrika (Afcon 2019) huko nchini Misri.
Akitoa maoni yake juu ya mashindano yanayoendelea nchini Misri, Mdau wa soka kutoka katika jiji la Dodoma, Shaban Juma alisema “nina imani na timu yetu ya Taifa kuwa itaifunga timu ya Kenya katika mchezo utakaochezwa tarehe 27 Juni, 2019”. Aliongeza kuwa Taifa stars inatakiwa kuishinda mechi hiyo kurudisha matumaini na moyo wa maelfu ya watanzania. Juma ambaye pia ni mchumi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma alisema kuwa Taifa stars ikifuzu kwa hatua inayofuata litakuwa ni jambo jema zaidi kwa afya ya soka nchini.
Akiongelea kichapo cha mabao 2-0 iliyokipata timu ya Taifa stars kutoka kwa timu ya Taifa ya Senegal (Lions of Teranga), Juma alisema kuwa uwezo wa timu ya Senegal ni mkubwa kuliko wa Tanzania. “Timu ya Senegal ni kubwa kuliko Tanzania na inauzoefu mkubwa na mechi za kimataifa. Shukrani kwa mechi yao tulifungwa magoli machache” alisema Juma.
Naye Afisa Habari katika halmashauri ya Jiji la Dodoma, Ramadhani Juma alisema kuwa timu ya Kenya inafungika. “Mpira wa Tanzania na Kenya utatawaliwa na kujuana zaidi” alisema Juma. Akiongelea kuiona nafasi ya Taifa stars kusonga mbele alisema kuwa nafasi hiyo ipo kwa sababu anatarajia timu ya Kenya kufungwa mabao mengi itakapokutana na timu ya Taifa ya Senegal, na hivyo Tanzania inaweza kusonga mbele kwa nafasi ya 'best loser' endapo itaifunga Kenya keshokutwa Alhamisi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.