MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kanda ya kati imefanya mafunzo kuhamasisha matumizi ya huduma za mtandao (broadband) kwa wadau wa huduma za mtandao, mafunzo haya yamefanyika leo katika ukumbi wa TCRA jijini Dodoma.
Akitoa salamu kwenye mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mkuu wa Kanda ya Kati Boniface Shoo amesema kuwa lengo la semina hiyo ni kuongeza matumizi na upatikanaji wa huduma bora za mtandao kwa wananchi, taasisi za serikali na watu binafsi.
Mafunzo hayo yametolewa kwa maafisa TEHAMA kutoka Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Halmashauri ya Mji Kondoa na Halmashauri za Wilaya ya Mpwapwa, Kongwa, Chamwino, Bahi, Chemba, na Kondoa. Aidha, kulikuwa na ushiriki wa watoa huduma za mtandao kutoka Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Vodacom, Tigo, Airtel na Halotel.
Akiwasilisha mada katika mkutano huo, Afisa kutoka TCRA Anania Mashenene amezitaja faida za matumizi na huduma za mtandao kuwa ni pamoja na kurahisisha na kutanua wigo wa biashara, kupunguza muda na gharama, kukuza ubunifu na uvumbuzi, urahisi katika upashanaji habari na kufika maeneo mengi kwa wakati, kupunguza mianya ya rushwa na kurahisisha utoaji huduma mbalimbali na uendeshaji wa shughuli serikalini.
Huduma za mtandao zinatumika katika mifumo ya taasisi za serikali na binafsi, huduma za kijamii kama vile shule, hospitali, mifumo ya biashara, mitandao ya kijamii, mifumo ya malipo ya ankara na mifumo ya ulinzi kama vile kamera za usalama (CCTV) amesema Mashenene.
Akizungumzia wajibu wa Serikali na hasa Halmashauri katika kukuza matumizi ya mtandao na utoaji wa huduma bora, Mashenene amesema halmashauri zina wajibu wa kuainisha maeneo yenye uhitaji wa mtandao, kutenga bajeti mahsusi kwa ajili ya TEHAMA, kutengeneza mifumo itakayosaidia katika kutoa huduma kwa wananchi ikiwemo elimu na afya.
Nao watoa huduma kwa upande wao walielezea huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi zao ikiwemo huduma za sauti na data kama vile mawasiliano ya simu, vituo vya kuhifadhia data (data center), huduma za simu bure (CUG), kutuma ujumbe mfupi kwa watu wengi (bulk sms), na matumizi ya mkongo wa taifa katika kutoa huduma hizo.
Washiriki walibainisha changamoto za upatikanaji wa mawasiliano katika baadhi ya maeneo ya Halmashauri zao na kupendekeza namna bora zitakazowezesha upatikanaji wa huduma bora kwa kutumia mtandao katika halmashauri zao.
Vile vile, Mashenene amesema kuwa TCRA itaendelea kuwahimiza watoa huduma kufikisha huduma za kimtandao kwenye maeneo ambayo huduma haipatikani au kuna upatikanaji hafifu.
Aidha, Serikali kupitia taasisi zake za TCRA na USCAF zitahakikisha uainishaji na ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya huduma za kimtandao katika maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara yanapewa kipaumbele ili kupata huduma hizo pia.
Washiriki wa semina pamoja na wawezeshaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania na wawakilishi wa watoa huduma wakiwa katika picha ya pamoja (picha ya juu na chini).
Mwakilishi kutoka Airtel Bi. Delphina Msuya akielezea huduma zitolewazo na kampuni ya Airtel wakati wa mafunzo kwa wadau wa huduma za mtandao.
Mwakilishi kutoka Tigo Bw. Delphina Msuya akielezea huduma zitolewazo na kampuni ya Airtel wakati wa mafunzo kwa wadau wa huduma za mtandao.
Mwakilishi kutoka Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) Bw. Deogratius Urassa akielezea huduma mbalimbali zitolewazo na TTCL wakati wa mafunzo kwa wadau wa huduma za mtandao.
Mwakilishi kutoka Kampuni ya Simu ya Vodacom Bw. Athumani Ngoma akielezea huduma mbalimbali zitolewazo na Vodacom wakati wa mafunzo kwa wadau wa huduma za mtandao.
Mwakilishi kutoka Kampuni ya Simu ya Halotel Bw. Steven Komu (Kulia) akifafanua juu ya huduma zitolewazo na Halotel wakati wa semina ya wadau wa huduma za mtandao.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.