Wadau wa mapambano dhidi ya ukatili kwa watoto katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kutumia vizuri rasilimali zilizopo kwa manufaa ya ulinzi na ukuaji wa mtoto.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la KISEDET, Nino Tragni ofisini kwake muda mfupi kabla ya kuanza kwa jukwaa la watoto la Halmashauri ya Jiji la Dodoma lililoandaliwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kushirikiana na wadau na kudhaminiwa na KISEDET leo.
Tragni alisema “jamii inatakiwa kuwa ‘pro active’ kutumia vizuri rasilimali kidogo zilizopo kwa manufaa ya ukuaji wa watoto”. Alishauri kuwa maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika yafanyike katika maeneo ambayo watoto wanatoka kuliko kupelekwa maeneo ambayo yana muingiliano wa shughuli nyingine za kijamii na uchumi jambo linaloondoa umakini wa maadhimisho hayo.
Akiongelea vitendo vya ukatili kwa watoto, Mkurugenzi huyo aliitaka jamii kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili. “Ni muhimu kutoa elimu hii katika shule kwa watoto wenyewe na walimu pia. Elimu hiyo iwawezeshe walimu kugundua viashiria vya ukatili kwa watoto mapema kabla havijatokea na kusababisha usumbufu kwa watoto”, alisema Tragni.
Mkurugenzi huyo aliipongeza serikali kwa kuajiri maafisa ustawi wa jamii wengi katika maeneo mbalimbali. “Serikali ipeleke fedha katika idara ya ustawi wa jamii na elimu ili maafisa hao waweze kutekeleza majukumu yao vizuri” alisisitiza Tragni. Aidha, aliwashauri maafisa ustawi wa jamii kutoka ofisini na kutembelea makao ya watoto na maeneo mengine ili kujadili changamoto zilizopo na kuzipatia ufumbuzi.
Nae mjumbe wa jukwaa la watoto katika Halmashauri ya jiji la Dodoma, Kaisi Omary alishauri kuwa watoto wasiteswe na kunyanyaswa. “Mimi nachowashauri msiwatese hawa watoto sababu watoto ni wakwetu sote. Tuwapende, tuwalinde tukiwaelekeza wanafuata kile tunachotaka. Pia waepuke makundi mabaya na matumizi ya vilevi kama kunywa pombe na kuvuta bangi. Kilevi kinamuaribu saikolojia na akili yake, anakuwa kila muda anawaza pombe na kuiba” alisema Omary. Akiongelea siku ya mtoto wa Afrika alisema kuwa siku hiyo inawapa fursa watoto kutaja mambo yanayowakera ili jamii iweze kuyatatua.
Maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika mwaka 2019, yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Mtoto ni msingi wa Taifa endelevu, tumtunze, tumlinde na kumuendeleza”. Maadhimisho hayo yanatanguliwa na shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na jukwaa la watoto linalofanyika katika makao ya watoto KISEDET na kilele chake kitafanyika kesho katika shule ya msingi Chang’ombe iliyopo Kata ya Chang’ombe jijini hapa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.