MKUU wa Wilaya ya Dodoma Christine Mndeme amesema wafanyabiashara ndogo waliozunguka eneo la bustani ya Uhuru katika Manispaa ya Dodoma wataondolewa na kuhamishiwa katika masoko ya Sabasaba na Bonanza ili eneo hilo libaki wazi kwa ajili ya kuupendezesha mji wa Dodoma na kuufanya uvutie zaidi ili kufikia lengo la kuboreshwa kwa bustani hizo.
Alitoa ahadi hiyo alipokuwa akifungua rasmi bustani hiyo leo Juni 5, 2017 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kilele cha Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya ‘Nyerere Square’ Manispaa ya Dodoma.
Bustani hiyo inahudumiwa na Benki ya Biashara ya Akiba (ACB) kwa makubaliano maalum na Manispaa ya Dodoma, ambapo meneja wa tawi la Benki hiyo John Magigita ameeleza kuwa changomoto kubwa ni kuwa bustani hiyo imezungukwa na wafanyabiashara ndogo hali inayopelekea kupoteza mvuto wake na kutoonekana vizuri.
Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede amesema Manispaa ya Dodoma itashirikiana na Ofisi ya Mkuu huyo wa Wilaya katika kuwahamisha wafanyabiashara hao na kuwatafutia nafasi katika masoko mengine baada ya soko la majengo kujaa hali iliyopelekea wao kupanga bidhaa zao katika viunga vya bustani hiyo.
Naye Afisa Mazingira na Usafishaji wa Manispaa ya Dodoma ambaye alimuwakilisha Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Godwin Kunambi katika Hafla hiyo fupi ya ufunguzi, alisema kuwa Manispaa imejipanga kuhakikisha mji wa Dodoma unakuwa katika hali ya usafi muda wote kwani tayari Dampo jipya la kisasa la kuzika taka lililopo katika eneo ya Chidaya limeshaanza kazi na kwamba watendaji wa Kata watashirikishwa kikamilifu katika kusimamia sheria za usafi na mazingira katika maeneo yao.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.