Afisa Masoko wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, James Yuna (pichani juu) amewataka wafanyabiashara jijini hapa kuhakikisha wanayatumia maeneo ya masoko yaliyotengwa na Halmashauri ya Jiji ipasavyo ili kuweza kuepukana na athari zinazoweza kujitokeza pindi wanapovamia maeneo yasiyo rasmi na kuyarasimisha kwa kufanyia biashara zao.
Yuna ameyasema hayo wakati akihojiwa kwenye kituo cha redio cha Dodoma FM katika kipindi cha Dodoma live, ambapo ametoa ufafanuzi juu ya masoko yaliyopo katika maeneo ya Jiji la Dodoma na namna ambavyo wafanyabiashara hawayatumii na badala yake kupanga bidhaa zao barabarani hali inayohatarisha usalama wao na bidhaa pia.
Afisa masoko huyo alisema Dodoma ni moja kati ya Halmashauri zenye miundombinu mizuri hasa upande wa masoko, ambapo karibia kila eneo kuna soko ambalo wafanyabiashara wanaweza kulitumia katika kujipatia kipato lakini hali imekuwa tofauti kwani badala ya wananchi kufuata mahitaji sokoni mahitaji yamekuwa yakiwafuata barabarani.
“Jiji la Dodoma lina Kata 41, mpango wa Jiji kila Kata inapaswa kuwa na soko na ni Kata chache ambazo bado hazina, tayari Halmashauri ilishatenga maeneo hayo, katikati ya mji tuna masoko 12 ambayo yanafanya vizuri na kuhudumia wateja wengi ikiwemo soko la Bonanza linalohudumia wananchi kwa upande wa matunda, mbogamboga, mahindi mabichi na samaki wabichi.
“Pia tunalo soko la Majengo ambalo ndio kongwe zaidi na mengineyo ambayo yanafanya kazi chini ya usimamizi wa ofisi ya Mkurugenzi, ambapo mfanyabiashara anatakiwa kuandika barua ya kuomba eneo na kisha atapatiwa majibu kama eneo lipo na atapewa, lakini kumekuwa na changamoto kubwa ya maeneo rasmi ya masoko kutokutumiwa na badala yake wanatumia kupanga biashara zao barabarani na kuathiri utendaji kazi wa maeneo hayo,” alisema Yuna.
Aidha ametoa ufafanuzi juu ya upangishaji wa vibanda vya biashara ambapo wengi wamekuwa wakifanya udalali na kuwatoza hela kubwa tofauti na ile iliyopangwa na Halmashauri, ametoa onyo kwa wale wote wenye tabia hiyo kuacha mara moja kwani kufanya vitendo hivyo ni kinyume na taratibu na endapo watabainika watachukuliwa hatua za kisheria.
“Ukipata eneo la kufanyia biashara fanya wewe mwenyewe na endapo utashindwa toa taarifa kwa mamlaka husika na libaki kuwa wazi ili mfanyabiashara mwingine anayehitaji kulitumia apatikane na apangishwe.
“Wafanyabiashara pia hakikisheni mnatoa taarifa sehemu husika endapo mtabaini kuna vitendo hivi vya udalali vinaendelea katika masoko yenu ili sisi tupate kuyafahamu, lakini endapo ninyi mtashindwa kuwa wakweli mnaokumbana na adha hii itakuwa ngumu kupatiwa msaada wa haraka,” alisema Afisa Masoko huyo.
Aidha alitoa wito kwa wafanyabiashara wote kuhakikisha wanayatumia masoko yaliyoko kwenye maeneo yao na kusisitiza kuwa wanaendelea kutoa elimu juu ya dhana ya utafutaji, na kuwahimiza kila mtu aendelee kuwajibika katika eneo lake na kuepukana na uvamizi wa maeneo yasiyo rasmi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.