Na. Faraja Mbise, DODOMA
Wafanyabiashara wameshauriwa kutumia haki yao ya msingi ya kikatiba kupiga kura kwa kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura ili waweze kupiga kura na kuwachagua viongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Ushauri huo ulitolewa na Meneja wa Kidia Vision Hotel, William Moshi alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa wafanyabiashara kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura ili kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa nje ya hoteli yake.
Moshi alisema kuwa anawahamasisha wananchi wa halmashauri ya jiji la Dodoma kujitokeza kushiriki zoezi la kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura. Kupiga kura ni haki ya msingi ya kikatiba. Wananchi watumie fursa hiyo kuchagua viongozi wa Serikali za Mitaa ili kuepukana na madhara yote yatakayojitokeza pindi wasipojiandikisha katika orodha ya wapiga kura na kushindwa kuwachagua viongozi bora.
“Nawasihi wakazi wote na wafanyabiashara wa Jiji la Dodoma na wakazi wengine wote, kujitokeza kwa wingi na kujiandikisha kutumia haki yao ya msingi ya kikatiba, kuchagua viongozi wao kwa ajili ya maendeleo yao na ya taifa. Hakuna mtu mwingine anayeweza kukuchagulia wewe kiongozi anaefaa bali ni wewe mwenyewe mkazi wa mtaa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla tujitokeze kwa wingi tukajiandikishe kwenye orodha ya wapiga kura” alisema Moshi.
Akiongelea uchaguzi wa viongozi bora, alisema kuwa wanachaguliwa na watu wenyewe kwa ajili ya maendeleo yao. “Hakuna mtu mwingine mwenye wajibu wa kukuchagulia kiongozi, bali ni wewe mfanyabiashara, mwananchi na mkazi wa kawaida kutumia nafasi hii ya kujiandikisha kwenye orodha ya wapiga kura ili uweze kuchagua kiongozi anaekufaa kwa ajili ya maendeleo yako na taifa lako” alisisitiza Moshi.
Akiongelea madhara ya mtu kupoteza sifa ya kuwa mpiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa alisema kuwa ni kutojiandikisha kwenye orodha ya wapiga kura. “Madhara ambayo yanatokana na kutojitokeza kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura, kwanza, hutoweza kupiga kura na kama hutoweza kupiga kura utakuwa umepoteza haki yako ya msingi ndani ya miaka mitano ya kumchagua kiongozi ambaye unaona anafaa. Madhara mengine utabaki unalalamika kuwa kiongozi ambaye yupo madarakani hafai, wakati ulipewa nafasi hukuitumia. Halmashauri ya Jiji la Dodoma takribani wiki mbili, tatu inatangaza kwenye magari ya matangazo wananchi wajitokeze kujiandikisha” alisisitiza Moshi.
Pia aliwashauri wananchi wenye sifa na vigezo vya kupiga kura na kuandikishwa kwenye orodha ya wapiga kura wajitokeze kwa wingi kabla zoezi halijaisha ili waweze kutumia haki yao ya msingi ya kuchagua na kuchaguliwa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. “Mpiga kura anapaswa awe ametimiza umri wa mika 18 na kundelea, anatakiwa awe na akili timamu ili aweze kutambua ni kiongozi gani anayeweza na kufaa kumuongoza, kiongozi gani anaweza kufaa kuwa chachu ya maendeleo katika nchi hii, awe mkazi wa mtaa husika, awe amejiandikisha katika orodha ya wapiga kura katika mtaa husika na awe ni raia wa Tanzania. ‘Serikali za Mitaa, Sauti ya Wananchi, Jitokeze Kushiriki Uchaguzi’
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.