Na. Dennis Gondwe, DODOMA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma kimewahakikishia wafanyabiashara wa Soko la Sabasaba kuwa hawataondolewa katika soko hilo hadi Mwezi Julai mwakani ili waendelee kutekeleza majukumu yao bila wasiwasi.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa katika mkutano wa hadhara na wafanyabiashara wa Soko la Sabasaba jijini Dodoma.
Kimbisa alisema “napenda kuwafahamisha kuwa hadi mwezi Julai mwakani hakuna mfanyabiashara atakayebughudhiwa hadi halmashauri itakapopata fedha za kuendeleza soko hilo. Halmashauri wakipata fedha hizo lazima tukae pamoja na kukubaliana wanaanza na jambo gani na kuendelea na jambo gani. Tunafahamu jiji mtajenga kwa awamu, mtashirikiana na uongozi wa soko ili kuhakikisha huduma zinakuwa bora”.
Akiongelea daladala kuingia katika Soko la Sabasaba, alisema kuwa soko hilo siyo stendi ya daladala. “Daladala zinapopaki kwa sasa si sawa. Daladala zilipo zitaua watoto wa shule na wagonjwa. Fanyeni haraka daladala zipite na kushusha na kupakia abiria katika Soko la Sabasaba hii siyo stendi. LATRA kaeni na uongozi wa soko kuhakikisha daladala zinapita hapa”.
Aidha, aliutaka uongozi wa soko kuwaondoa wafanyabiashara wanaofanya biashara kwa kutandaza hadi eneo ambalo daladala zinapita. Alimtaka Mkuu wa Wilaya ya Dodoma kuhakikisha askari Polisi wanakuwepo muda wote ili daladala zisitumie muda mrefu kusubiria abiria.
Mfanyabiashara katika Soko la Sabasaba, Madimilo Mbogoni alisema kuwa walikuwa na hofu ya kuondolewa katika soko hilo. “Tunamshukuru Mwenyekiti wa CCM kwa kufika kuongea na sisi wafanyabiashara wa Soko la Sabasaba. Sasa tulikuwa na hofu kubwa kuhusu kuondolewa katika maeneo haya tumeteseka kwa muda mrefu kujua hatima yetu. Lakini leo tumepata ufumbuzi na kweli tunawashukuru viongozi wote walioshiriki mpaka kuhakikisha tumefikia hapa. Hofu yetu imetutoka na tunamshukuru Mungu” alisema Mbogoni.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa alipokuwa akingea katika mkutano wa hadhara na wafanyabiashara wa Soko la Sabasaba jijini Dodoma leo tarehe 24/08/2023.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.