Wafanyabiashara wa Soko Kuu Majengo katika eneo la Stockyard Jijini Dodoma ambao wamekuwa wakiuza matunda na mboga mboga kwenye eneo la wazi na hivyo kuathiriwa na jua kali na mvua, wamekuwa na furaha kubwa baada ya kukabidihiwa vifaa vya ujenzi wa paa la Soko eneo la Stock Yard na hivyo kuanzisha mchakato wa ujenzi ikiwa ni utekekelezaji wa ahadi iliyotolewa mwaka 2015 na Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mheshimiwa Anthony Mavunde. Soko la Majengo lilizinduliwa mwaka 1996.
Akitoa shukrani kwa niaba ya wafanyabiashara wengine Mama Esther Mazengo amemshukuru Mbunge Mhe. Mavunde, Diwani Mhe. Msinta Mayaoyao na Halmashauri ya Jiji kwa kutatua kero hii ambapo wamekaa eneo hilo la wazi kwa muda mrefu na bidhaa zao nyingi kuathiriwa na jua na mvua na hivyo kuwasababishia hasara kila mara.
Akihutubia wananchi hao, Mhe. Mavunde amemshukuru Mkurugenzi wa Jiji Ndugu Godwin Kunambi kwa ushirikiano mkubwa alioutoa wa kiasi cha shilingi 50,000,000 (milioni hamsini) kupitia Halmashauri ya Jiji kwa ununuzi wa mabomba na mabati pamoja na Kampuni ya Dragon kwa kuchangia mabati 200 kufuatia maombi aliyoyawasilisha, aidha alitumia fursa hiyo kumpongeza Diwani wa Kata ya Majengo Mheshimiwa Msinta Mayaoyao kwa ufuatiliaji na usimamizi makini.
“Nafahamu kuna changamoto nyingi sana mnazokumbana nazo, lakini kwa ushirikiano wetu tutazitatua. Nipende kuishukuru Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kushirikiana nasi katika kuboresha miundombinu ya soko letu.
“Leo tumeleta na tumekabidhi mabati 400, nguzo 50 kutoka katika kampuni la Dragon na kampuni hii imechangia mabati 200 wakiwa na lengo la kuunga mkono juhudi za kuboresha miundombinu ya soko hili la Majengo,” alisema Mavunde.
"Tunategemea baada ya kukamilika paa hili wafanyabiashara wengi zaidi watapata nafasi ya kuuza bidhaa zao kwa nafasi na katika mazingira salama, na mimi kwa nafasi yangu nitawatafutia meza za kisasa za kuuzia bidhaa zenu kama nilivyofanya kwenye soko la Chang'ombe na Mavunde Garden" alisema Mavunde.
Naye Afisa Masoko wa Jiji Bwana James Yuna kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji, ameahidi kusimamia uboreshwaji wa masoko yote ya Jiji la Dodoma ili yaendane na kasi ya ukuaji wa Jiji na kutengeneza mazingira nadhifu ya kufanya biashara.
Mheshimiwa Anthony Mavunde akiongea na hadhira ya wafanyabiashara wa Soko kuu la Majengo eneo la Stock Yard wakati alipofanya ziara ya kutembelea soko hilo na kutoa msaada wa vifaa vya ujenzi wa paa eneo la Stock Yard. Kushoto kwa Mhe. Mavunde ni Diwani wa kata ya Majengo Mhe. Msinta Mayaoyao na wa kwanza kushoto ni Afisa Masoko wa Jiji la Dodoma James Yuna.
Diwani wa Kata ya Majengo Mheshimiwa Msinta Mayaoyao akiongea na wafanyabiashara wa soko la Majengo, kulia kwake ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini Mhe. Anthony Mavunde.
Mhe. Anthony Mavunde (mwenye kofia ya pama) na Diwani wa Majengo Msinta Mayaoyao (aliyeshika mic kushoto) kwa pamoja wakikabidhi mabati kwa ajili ya ujenzi wa paa sokini Majengo.
Wafanyabiashara wa Soko Kuu la Majengo wakimpongeza mbunge wao Mhe. Anthony Mavunde kwa kutekeleza ahadi aliyoitoa mwaka 2015 wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.
Wafanyabiasha wa soko la Majengo wakishangilia hotuba ya Mhe. Anthony Mavunde.
Eneo la Stock Yard ambalo litawekewa paa ili kuondoa adha ya jua na mvua kwa wafanyabiashara wa Soko kuu la Majengo eneo hilo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.