WAFANYABIASHARA wa Soko la Matunda, Samaki wabichi na mbogamboga la Bonanza katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kushirikiana na Jiji la Dodoma na pia kuacha kufanya biashara kwa mazoea, badala yake waboreshe ili waweze kufikia malengo na kujiinua kiuchumi.
Aidha, wametakiwa kutumia fursa za ukuaji wa kasi wa Jiji la Dodoma na ongezeko kubwa la idadi ya wakazi kulikosababishwa na uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma. Hivi sasa kuna idadi kubwa ya watu wanaoweza kununua bidhaa zao mbalimbali.
Ushauri huo ulitolewa na Mwenyekiti wa soko hilo, Marwa Mabucha, wakati akizungumza na wafanyabiashara baada ya kuchaguliwa kwenye uchaguzi mkuu wa viongozi wa soko hilo uliofanyika jijini Dodoma.
Vilevile, aliwataka wafanyabiashara hao kuachana na biashara za mazoea ambazo hazina tija, badala yake wafanye kwa malengo ya kuinua mitaji yao ili waweze kupata mikopo ambayo itawawezesha kukabiliana na wingi wa wateja wanaowahudumia.
Mabucha alisema bila wafanyabiashara kubadilisha mtizamo wao wa kizamani wa kufanya biashara kimazoea kwa idadi ile ile ya watu wakati ikiwa Manispaa hawataweza kujiinua kiuchumi na kuendana na mahitaji ya sasa katika Jiji la Dodoma.
Mwenyekiti huyo ambaye alichaguliwa kwa kura 196, aliwataka wafanyabiashara hao kushirikiana kwa pamoja na Halmashauri ya Jiji ili kuweza kuboresha soko hilo kwenye miundombinu.
Kwa upande wake mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Goya Magwai, aliutaka uongozi uliochaguliwa kushirikiana na wafanyabiashara hao pamoja na Jiji ili waweze kuwahudumia wateja wao na kutatua changamoto zilizopo.
Katika uchaguzi huo viongozi wengine waliochaguliwa ni pamoja na Makamu Mwenyekiti Fortunatus Keleta, aliyechaguliwa kwa kura (119), Katibu wa soko Dickson Mwesigwa (209), Katibu Msaidizi Hamisi Mbula (105) na Mtunza Hazina Elias Manikulu (286).
Chanzo:www.ippmedia.com
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.