WAFANYABIASHARA jijini Dodoma wametakiwa kufanya biashara zao kwa kuzingatia masharti ya leseni zao ili kuepuka migongano isiyo ya lazima na mamlaka na kulinda hadhi ya Makao Makuu ya Nchi.
Kauli hiyo Imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge katika kikao chake na wafanyabiashara wamiliki wa baa na nyumba za kulala wageni katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Dkt. Mahenge amesema kuwa wafanyabiashara wanatakiwa kufanya shughuli zao kwa kuzingatia masharti yaliyo katika leseni zao za biashara. “Kama mfanyabiashara kapewa leseni ya ‘grocery’ afanye kazi ya ‘grocery’ na siyo kazi ya baa. Wafanya biashara hakikisheni mnazingatia masharti ya leseni mlizonazo” amesema Dkt. Mahenge.
Mkuu wa mkoa aliongelea suala la upigaji muziki kinyume na sheria na kusababisha kero kwa watu wengine. “Tumekuwa tukipokea malalamiko ya ukiukaji wa sheria za leseni kwa kupiga muziki kwa sauti ya juu sana na kusababisha kero kwa watu wengine. Kutokana na kelele za muziki huo, watu wanashindwa kulala na kupumzika, watu wanashindwa kufanya kazi zao kwa kiwango kinachokubalika kutokana na kutokupumzika na kusababisha ufanisi kupungua” alisema Dkt. Mahenge.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alisema kuwa halmashauri hiyo iliandaa mpango kabambe wa miaka 20 ukionesha uendelezaji ardhi wa jiji hilo. Mpango huo umeainisha maeneo ya viwanda, makazi, taasisi, elimu na makazi na biashara kwa lengo la kuepuka muingiliano wa matumizi ya ardhi. “Tumetenga maeneo hayo kwa lengo la kujenga mji safi na salama, unaofikika na shindani. Ninyi mpo katika eneo la huduma ya makazi na biashara. Tatizo mmeanza kukiuka matakwa ya leseni zenu. Tulikupa leseni ya ‘grocery’ sasa unaendesha baa na kupiga muziki kwa sauti ya juu” alisema Mkurugenzi Mafuru.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dkt. Binilith Mahenge (wa pili kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru (aliyesimama kulia) akitoa maelezo kuhusu Jiji lilivyojipanga kuhakikisha wafanyabiashara wanafanya shughuli zao kwa mujibu wa mpango wa matumizi bora ya ardhi Jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru akifafanua jambo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na wafanyabiashara katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.