Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka wagombea wote ambao hawajaridhishwa na uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa waweke pingamizi ndani ya siku 2 kuanzia leo tarehe 08 - 09/11/2024.
Amesema hayo wakati akiongea na vyombo vya habari kuhusu uteuzi wa wagombea katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma
“Kama mnavyojua, leo ni siku muhimu ya uteuzi wa wagombea kwaajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mujibu wa Kanuni ya 18 ya Tangazo la Serikali Na. 571, 573, 574, pamoja na Kanuni ya 17 ya Tangazo la Serikali Na. 572 yote ya tarehe 12 Julai 2024.”
“Kanuni hizi zinamtaka Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi kufanya uteuzi wa wagombea leo tarehe 8 Novemba, 2024, kuanzia saa mbili kamili asubuhi hadi saa kumi kamili jioni. Mara baada ya uteuzi kukamilika, majina ya wagombea wenye sifa na wale ambao hawajakidhi vigezo vya kugombea yatabandikwa hadharani ili umma uweze kuyapata wakiwemo wagombea wenyewe”.Aliongeza Mhe. Mchengerwa.
Ameendelea kueleza kuwa kwa mujibu wa Kanuni hizo mtu yeyote aliyeomba kuteuliwa kuwa mgombea au mgombea ambaye hakuridhika na uamuzi uliotolewa na Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, anaweza kuwasilisha pingamizi na kumuomba Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi kupitia upya uamuzi uliofanyika ili amteue kuwa mgombea au atengue uteuzi anaoupinga.
Amesema kwamba pingamizi hili linaweza kuwasilishwa kwa maandishi ndani ya siku mbili tangu uamuzi au uteuzi ulipofanyika. Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi atalishughulikia pingamizi hilo na kutoa uamuzi ndani ya siku mbili tangu alipolipokea.
“Hivyo, kwa mujibu ya kanuni hizi, kuanzia leo tarehe 8 na kesho tarehe 9 Novemba 2024, kwa mgombea yeyote ambaye hatoridhika na uamuzi wa Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi kuhusu uteuzi, anapaswa kutumia nafasi ya siku hizi mbili ili malalamiko yake yaweze kufanyiwa kazi kwa mujibu wa Kanuni’.Alisisitiza
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.