Wagonjwa wa Sikoseli nchini wamepewa unafuu wa gharama na upatikanaji wa dawa baada ya Serikali kupitia Wizara ya Afya kuweka mikakati madhubuti inayolenga kuboresha huduma kwa wagonjwa hao.
Hayo yamesemwa leo mbele ya Waandishi wa Habari jijini Dodoma na Kaimu Mkurugenzi wa huduma za Tiba wa Wizara Afya Dkt. James Kiologwe aliyemwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali katika kilele cha maadhimisho ya mwezi wa Sikoseli duniani.
Dkt. Kiologwe amesema miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na Serikali ni pamoja na kujumuisha Sikoseli katika Mpango Mkakati wa Taifa wa pili wa magonjwa yasiyoambukiza wa mwaka 2016-2020 na kuhakikisha kliniki za wagonjwa wa Sikoseli zinaanzishwa katika mikoa yote nchini ikiwa ni pamoja na upatikanaji rahisi wa dawa ya Hydroxyurea ambayo itaingizwa katika muongozo wa matibabu na kuwekwa katika orodha ya dawa zinazolipiwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Aidha, Dkt. Kiologwe amesema Serikali itahakikisha kwamba vipimo vya papo kwa papo (Sickle Scanner) na dawa ya HU vinaingia kwenye Kinadi cha bei cha Bohari ya Dawa (MSD Price Catalogue).
Pamoja na hayo Dkt. Kiologwe amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaendelea kuielimisha jamii ili kuwa na uelewa wa pamoja juu ya ugonjwa huu ambapo inatarajia kwa kiasi kikubwa itapunguza na hatimaye kuondoa unyanyapaa kwa wagonjwa wenye Sikoseli.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya duniani (WHO) inaonesha kila siku zaidi ya Watoto 1,000 huzaliwa na Sikoseli huku Tanzania takwimu zinaonesha zaidi ya Watoto 11,000 huzaliwa na ugonjwa wa Sikoseli kila mwaka, sawa na kusema Watoto 8 kati ya 1,000 uzaliwa na ugonjwa huu.
Maadhimisho ya mwezi wa Sikoseli hufanyika mwezi Septemba kila mwaka duniani kote na mwaka huu yalikua na kaulimbiu inayosema “Ijue Sikoseli, epuka unyanyapaa”.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.