WAWEKEZAJI wameshauriwa kuwekeza katika maeneo ya uzalishaji, usindikaji na uuzaji mazao ya kilimo ili kuongeza tija katika sekta hiyo.
Ushauri huo ulitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alipokuwa akieleza fursa za uwekezaji katika kuzalisha, kusindika na kuuza mazao ya kilimo katika kongamano la uwekezaji lililofanyika katika ukumbi wa ‘Dodoma Convention Centre’ jijini hapa jana.
Kunambi alisema kuwa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, ipo fursa ya kuwekeza katika kuzalisha, kusindika na kuuza mazao ya kilimo. Maeneo ya fursa hizo aliyataja kuwa ni kuzalisha Zabibu kibiashara, viwanda vya mvinyo, na sharubati ya Zabibu na kusindika mbogamboga. Maeneo mengine aliyataja kuwa ni fursa katika kuanzisha viwanda vya kusindika mbegu za mafuta na kuzalisha vyakula vya mifugo. Kuwekeza katika maeneo hayo, kutaongeza tija kwa wakulima na ajira kwa vijana na kina mama kupitia sekta hiyo, aliongeza.
Kongamano la uwekezaji ngazi ya Mkoa limefanyika kwa siku mbili katika Halmashauri ya jiji la Dodoma likihudhuriwa na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi waliopata fursa ya kujadili fursa za uwekezaji na kutembelea maeneo mbalimbali yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji na miradi mikubwa ya uwekezaji.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.