Serikali imetoa fursa kwa wanafunzi waliofaulu Kidato cha Nne mwaka 2018 na wanaotegemea kujiunga na Kidato cha Tano pamoja na vyuo kwa Mwaka 2019 kubadilisha Tahsusi(Combination).
Akitoa taarifa kwa vyombo vya Habari Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mheshimiwa Selemani Jafo amesema, Serikali ya Awamu ya Tano inawapa wahitimu hao fursa ya kufanya mabadiliko ya machaguo ya Tahasusi (Combination) na kozi mbalimbali walizozichagua kwenye fomu ya "F4-Selform".
Ameongeza kuwa fursa hii itawawezesha wanafunzi kurekebisha machaguo yao kulingana na ufaulu waliopata kwenye matokeo ya Kidato cha Nne 2018 yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani Tanzania, NECTA.
“Kwa mara ya kwanza Wanafunzi watakuwa na uwezo wa kubadili machaguo au kuchagua kutoka Kidato cha Tano kwenda Chuo au Chuo kwenda Kidato cha Tano kwa kadiri ya mahitaji yake na jinsi alivyofaulu mitihani yake” amesema Jafo.
Unajua wanafunzi hujaza Fomu za "F4-Selform" kabla ya kufanya mitihani, sasa matokeo huweza kuja tofauti na vile alivyojaza lakini mwanafunzi huyo amefaulu, hivyo ni wakati sasa kwa kubadilisha machaguo kwa kadiri ya ufaulu wake na anavyopendelea mwenyewe, alisisitiza Jafo.
Aidha Waziri ameongeza kuwa "Ofisi yangu imetoa fursa hii kwa wahitimu kubadili machaguo yao ili kutoa mwanya zaidi kwa mwanafunzi kusoma fani au Tahasusi itakayomuandaa kuwa na utaalam fulani katika maisha yake ya baadaye kwa namna ambayo anatamani yeye mwenyewe au kwa kushauriwa na wazazi au walezi wake; Hii ni kutokana na ukweli kwamba baadhi ya wanafunzi hawakujaza kwa uhakika Tahasusi au Kozi zao kutokana na kutokuwa na uhakika wa ufaulu katika masomo yao.
Ameongeza kuwa zoezi la awali la kuingiza taarifa zilizo kwenye “Selform” za wanafunzi kwenye kanzidata ya Ofisi ya Rais - TAMISEMI, kama zilivyojazwa wakiwa shuleni kabla ya kuhitimu limekamilika na sasa wanafunzi wataweza kufanya mabadiliko kwa njia ya mtandao (online) na baada ya wanafunzi kufanya marekebisho yao, kanzidata hii ndiyo itakayotumika kuwachagua na kuwapangia kidato cha Tano na Kozi za Vyuo.
Waziri Jafo amewakumbusha wahitimu wote kuwa, endapo wanapenda kurekebisha machaguo ya Tahasusi na Kozi au kuhama kutoka Chuo kwenda Kidato cha Tano kulingana na ufaulu wao katika masomo wanatakiwa kuingia kwenye mfumo wa Selform unaopatikana katika anuani ya www.selform.tamisemi.go.tz na maelekezo ya jinsi ya kufanya mabadiliko watayapata kwenye video ya mafunzo inayopatikana kwenye tovuti ya TAMISEMI www.tamisemi.go.tz. Wanafunzi wanaweza pia kupata maelekezo kwa kusoma Muongozo wa Mwanafunzi katika Mfumo wa Selform namna ya Kuingia na Kubadilisha Machaguo. Bofya hapa kusoma: Muongozo wa Namna ya Kubadili Machaguo - Selform.pdf
Pia amefafanua kuwa Ili mhitimu aweze kuingia kwenye mfumo itabidi kutumia namba ya mtihani wa kuhitimu Kidato cha Nne mwaka 2018, jina lake la mwisho, mwaka wa kuzaliwa na alama ya ufaulu aliyopata kwenye somo atakaloulizwa na mfumo au swali lolote atakaloulizwa.
Zoezi hili la kubadilisha Tahasusi litafanyika kuanzia tarehe 01/04/2019 hadi tarehe 15/04/2019.
Chanzo: Tovuti ya OR-TAMISEMI (www.tamisemi.go.tz)
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.