RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ameitaka Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kifanyia kazi taarifa ya Mbionza Mwenge wa Uhuru na kuwachukulia hatua stahiki wale watakaobainika kuhusika na ubadhilifu katika miradi iliyotajwa kuwa na kasoro.
Mhe. Rais Samia, amesema hayo leo tarehe 14 Oktoba, 2021 wakati akihutubia katika kilele cha maadhimisho ya Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru, Kumbukizi ya miaka 22 ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere na Wiki ya Vijana yaliyofanyika katika viwanja vya Magufuli wilayani Chato Mkoani Geita.
Amesema haiwezekani kufikia maendeleo kama taifa litaendelea kkuwa na vitendo va rushwa na ufisadi, kwani vitengo hivyo ni chanzo cha ukiukwaji wa haki za wananchi, kuwepo kwa mikataba mibovu na ukiukwaji wa taratibu za ujenzi katika miradi ya maendeleo.
Aidha, Mhe. Rais Samia amesema amekuwa akijiuliza kwa nini viongozi wa maeneo ambayo miradi iliyokutwa na dosari ikiwa ni pamoja na Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Maofisa TAKUKURU na viongozi wa vyombo vya ulinzi ya usalama wapo lakini wanasubiri mpaka wakati wa mbio za Mwenge wa Uhudu zipite ndipo wabaini dosari za miradi hiyo.
Mhe. Rais Samia ametoa tahadhari kwa miradi inayokwenda kutekelezwa kwenye Mpango wa Maendeleo kwa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 kuwa lisijitokeze suala la ubadhilifu na kuwa atasimama imara kufuatilia utekelezaji wa miradi hiyo na miradi mingine.
Pia, Mhe. Rais Samia amewataka viongozi katika maeneo utakapopita Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2022 kuhakikisha idadi ya miradi yenye dosari inapungua.
Akizungumza juu ya kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere, amesema Serikali itaendelea kumuenzi Baba wa Taifa, kutokana na ujasiri aliokuwa nao ukiwemo ushupavu wa kuitumikia nchi yake.
Kuhusu sekta ya afya, Mhe. Rais Samia amesema bado hali sio nzuri kutokana na kuongezeka kwa maradhi yasio ya kuambukiza yakiwemo ya shinikizo la damu, Kisukari, Malaria pamoja na janga la UVIKO 19, jambo ambalo ni vyema kwa vijana wa Tanzania kuendelea kuchukua tahadhari ya maradhi hayo.
Mhe. Rais Samia, amewataka wnanchi kujikinga na UVIKO 19 kwa kuona umuhimu wa kuchanja kwani Serikali tayari imeshasambaza chanjo na kuwaasa vijana kuacha kutumia dawa za kulevya kutokana na athari zake kwa afya.
Mwenge huo wa Uhuru umetembelea, kukagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi 1,067 yenye thamani ya Zaidi ya Shilingi Trilioni 1.2 kutoka sekta za maji, nishati, afya, kilimo, uvuvi, mifugo na miundombinu.
Mapema alipowasili Wilayani Chato, Mhe. Rais Samia alizuri na kuweka shada la maua katika kaburi la aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli nyumbani kwako Chato mkoani Geita.
Maadhimisho ya kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru zimefanyika Wilaya ya Chato Mkoani Geita ili kumuenzi aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.