Na. Faraja Mbise, DODOMA
Wajasiriamali kutoka kata za pembezoni za Hombolo Makulu, Ipala, Mbalawala, Chihanga na Mnadani katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wamenufaika na mradi wa nishati jadidifu kwa matumizi ya uzalishaji uliolenga kuimarisha na kuboresha miradi ya wajasiriamali wa pembezoni.
Hayo yalisemwa na Afisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Santiel Mmbaga wakati wa mkutano na wadau mbalimbali wenye lengo mahususi la utoaji taarifa ya utekelezaji wa mradi wa matumizi ya nishaji jadidifu kwa matumizi ya uzalishaji kwa mwaka 2022 hadi 2024 katika ukumbi wa Maktaba ya Mkoa wa Dodoma.
Mmbaga alisema “halmashauri imeweza kunufaika sana na miradi hii ya Kakute ambayo imetufungia nishati hii jadilifu kwenye maeneo ya pembezoni, kwasababu wananchi wetu walikuwa wanahitaji huduma, walikuwa wanafanya kilimo, walikuwa wanachajisha simu lakini sio kwa kiwango hicho. Lakini saizi kilimo kilichokuwa kinafanyika kwa udogo sasa hivi kinafanyika kwa ukubwa zaidi kwasababu ya nishati ambayo Shirika la Kakute limeweza kuwafungia wananchi wetu. Kwahiyo, kama halmashauri tunaona wananchi wetu wameweza kuongeza kipato kutoka hali ya chini kwenda ya juu kidogo kulingana na hii nishati jadidifu. Kwahiyo, tunaendelea kuwashukuru sana na kuwakarisbisha ili tuendelee kufanya kazi kwa ushirikiano”.
Akizungumzia maendeleo ya wananchi katika jamii, aliishukuru serikali na Shirika la Kakute Projects kwa uwezeshaji walioufanya katika kata hizo kwasababu mradi umesaidia kuinua kipato cha mwananchi mmoja mmoja na jamii kwa ujumla. “Tunashukuru sana kwasababu wananchi wetu wameweza kupata maendeleo, wengine wameweza kupeleka watoto shule, wengine walikuwa hawana umeme wameweza kupata umeme ina maana watoto watasoma, watafaulu vizuri. Kwahiyo, tunaendelea kutoa shukrani zetu kwa serikali na Shirika la Kakute Projects, tuendelee kushirikiana ili tuweze kuinua wananchi wetu” alisema Mmbaga.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Mbalawala, Hessein Karume aliipongeza serikali kwa kuruhusu wadau mbalimbali kuunga mkono harakati za maendeleo ya jamii na kueleza namna ambavyo Kata ya Mbalawala imenufaika na mradi wa nishati jadidifu kwa ajili ya uzalishaji. “Shirika hili la Kakute Projects katika Kata ya Mbalawala, limewezesha wajasiriamali watatu na wajasiriamali hao wameleta mchango mkubwa sana katika Kata ya Mbalawala. Kwa mfano kuna sehemu ya kuchajishia simu, kuna uzalishaji wa kuku na kutotolesha kuku, hii yote ni miradi iliyowezeshwa na Kakute Projects. Pia watu wa Mbalawala wameweza kuwa na sehemu ya kukutana pamoja kwa mfano, mmoja wa wajasiriamali ana kituo cha kuonesha mpira na kuchajisha simu, na kimsingi tunaweza kusema kwamba, tumepata maendeleo makubwa ya kuonekana kupitia wajasiriamali hao. Kwahiyo, naipongeza serikali kwa kuwaruhusu wadau kama hawa kuweza kuja na kuunga mkono harakati za maendeleo” alisema Karume.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa DOM Energy Solutions and Designing Ltd, Anthony Machai, ambae ni msambazaji wa teknolojia katika mradi huu alipongeza juhudi za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kampeni ya kutokomeza matumizi ya nishati chafu na hivyo kumuunga mkono katika kusambaza teknolojia ambayo ni rahisi kwa wajasiriamali wa baadhi ya kata zilizopo jijini Dodoma kwa kushirikiana na Kakute Projects. “Tunajishughulisha na ufungaji wa mitambo ‘solar’ mbalimbali katika Jiji la Dodoma na Tanzania nzima. Ukiangalia kwa sasa hivi pia rais wetu yupo kwenye mchakato wa kuhakikisha wananchi kwa asilimia kubwa tunatumia nishati safi ambayo inatunza mazingira. Na sisi kama wadau wa nishati, tunampongeza kwa jitihada nyingi sana anazozifanya kutafuta wafadhili wengi watakaoiwezesha jamii yetu kupata nishati hii ambayo ni rahisi na kila mmoja anaweza akamudu” alisema Machai.
Kwa upande wake mjasiriamali Lucas Japhet, aliipongeza serikali kwa kuwaletea wadau ambao wamekuwa ni chachu kubwa sana katika kukuza biasahara zao na kuyafikia malengo kwa teknolojia nzuri walizowekewa. “Nimefungiwa mtambo wa ‘solar’ na umenirahisishia mimi kufanyakazi zangu kwa uhuru zaidi na kwa wepesi zaidi na mpaka sasahivi kuna mafanikio mazuri nimeyafikia na kikubwa ninafanya kazi kwa urahisi zaidi bila shida yoyote. Niishukuru serikali yetu ya Tanzania kwa kutuletea wadau kama hao wanaotuwezesha sisi wajasiriamali kupata nishati na hata kwa jamii pia” alisema Japhet.
Mradi wa nishati jadidifu kwa matumizi ya uzalishaji Dodoma ulianzishwa mwaka 2022 na kuweza kuzifikia kata tano ambazo ni Mbalawala, Chihanga, Hombolo Makulu, Mnadani pamoja na Ipala na kuwafikia wajasiriamali 15 ambao walipatiwa mitambo ya kuendesha biashara zao za uzalishaji.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.