Na. Faraja Mbise, DODOMA
WAJASILIAMALI katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wamehimizwa kurasimisha biashara zao kwa lengo la kuwa na wigo mkubwa wa kuweza kukopa katika taasisi za kifedha kwa sababu watakuwa wanatambulika kwa mujibu wa sheria.
Hayo yalisemwa na Katibu Mtendaji wa Shirika Kakute Projects, Livinus Manyanga alipokuwa akizungumza na wanufaika wa mradi wa nishati jadidifu, wadau wa serikali, viongozi wa sekta ya biashara na wazalishaji wa teknolojia katika mkutano wa wadau wa mradi wa nishati jadidifu kwa matumizi ya uzalishaji uliofanyika katika ukumbi wa Maktaba ya Mkoa uliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
“Tumejaribu kufanya kazi kwa karibu sana na vile vikundi ambavyo vimekopeshwa mikopo na halmashauri tofauti na hii misaada ambayo tumeitoa sisi, inaonesha wazi kwamba changamoto namba moja ni kwamba, mjasiriamali mdogo mpaka aweze kurasimisha biashara yake ni hatua ndefu na hawapendi kuchukua hatua ndefu kiasi hicho. Pia nidhamu ya matumizi ya pesa, kujua hii pesa imetoka wapi na inatakiwa kupelekwa wapi inakuwa ni ngumu kidogo. Tunazidi kusisitiza, uwekaji wa kumbukumbu, mpango wa biashara na kurasimisha biashara ni vitu vya msingi sana” alisisitiza Manyanga.
Akiongelea suala la teknolojia katika mradi, alisema kuwa wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwafikia walengwa na imesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha biashara zao. “Teknolojia imetengenezwa vizuri na inaonesha muelekeo wa kuwaongezea uzalishaji na pia kuboresha maisha yao kwa ujumla” alisema Manyanga.
Kuhusu suala la wadau wa kifedha, alisema mradi unashirikiana na taasisi mbalimbali za kifedha ili kuwasaidia wajasiriamali wadogo wadogo katika kata zilizopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa lengo la kuboresha miradi na kuimarisha usambazaji wa teknolojia. “Mradi unalenga kuwashirikisha wajasiriamali na wadau wa fedha kama SACCOS, VICOBA pamoja na Benki. Pamoja na mafunzo tuliyowapatia wajasiriamali waliopo maeneo ya pembezoni, uelewa wao ni wa taratibu, wanafahamu kila kitu lakini kutekeleza ni taratibu” alisema Manyanga.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa DOM Energy Solutions and Designing Ltd, Anthony Machai, ambae ni msambazaji wa teknolojia katika mradi huu alipongeza juhudi za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kampeni ya kutokomeza matumizi ya nishati chafu na hivyo, kumuunga mkono katika kusambaza teknolojia ambayo ni rahisi kwa wajasiriamali wa baadhi ya kata zilizopo jijini Dodoma kwa kushirikiana na Kakute Projects.
“Tunajishughulisha na ufungaji wa mitambo ya ‘solar’ mbalimbali katika Jiji la Dodoma na Tanzania nzima. Ukiangalia kwa sasahivi pia rais wetu yupo kwenye mchakato wa kuhakikisha wananchi kwa asilimia kubwa tunatumia nishati safi ambayo inatunza mazingira. Na sisi kama wadau wa nishati, tunampongeza kwa jitihada nyingi sana anazozifanya kutafuta wafadhili wengi watakaoiwezesha jamii yetu kupata nishati hii ambayo ni rahisi na kila mmoja anaweza akamudu” alisema Machai.
Kwa upande wake mjasiriamali, Lucas Japhet ameipongeza serikali kwa kuwaletea wadau ambao wamekuwa ni chachu kubwa sana katika kukuza biasahara zao na kuyafikia malengo kwa teknolojia nzuri walizowekewa. “Nimefungiwa mtambo wa ‘solar’ na umenirahisishia mimi kufanyakazi zangu kwa uhuru zaidi na kwa wepesi zaidi na mpaka sasahivi kuna mafanikio mazuri nimeyafikia na kikubwa ninafanya kazi kwa urahisi zaidi bila shida yoyote. Niishukuru serikali yetu ya Tanzania kwa kutuletea wadau kama hawa wanaotuwezesha sisi wajasiriamali kupata nishati na hata kwa jamii pia” alisema Japhet.
Mradi wa nishati jadidifu kwa matumizi ya uzalishaji Dodoma ulianzishwa mwaka 2022 na kuweza kuzifikia kata tano ambazo ni Mbalawala, Chihanga, Hombolo Makulu, Mnadani pamoja na Ipala na kuwafikia wajasiriamali 15 ambao walipatiwa mitambo ya kuendesha biashara zao za uzalishaji. Pia ulilenga kuimarisha na kuboresha miradi ya wajasiriamali wa pembezoni iwe na tija zaidi kwa kuunda ushirikiano kati ya wasambazaji wa suluhisho za teknolojia ya nishati jadidifu na kujenga msingi wa maendeleo endelevu kwa kushirikiana na viongozi wa serikali ngazi ya kata na wadau wengine wa maendeleo.
MWISHO
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.