WAJASIRIAMALI nchini wamekumbushwa kuwa wanawajibu wa kuwatafuta wanufaika wa bidhaa zao sehemu mbalimbali ili waweze nunua bidhaa hizo tofauti na dhana iliyozoeleka ya kukaa wakisubiri na kulalamikia soko.
Kauli hiyo ilitolewa na Afisa uendeshaji biashara wa Shirika la Kuhudumia Viwanda vidogo (SIDO) Mkoa wa Dodoma, Crispin Kapinga alipokuwa akielezea wajibu wa wajasiriamali katika kujitangaza na kutafuta masoko katika banda la SIDO kwenye maonesho ya Nanenane, Nzuguni jijini Dodoma.
Kapinga alisema “kilio kikubwa cha wajasiriamali ni soko, sasa tumekuja kuwaonesha kuwa soko siyo tatizo. Tatizo ni sisi wenyewe wajasiriamali kwa sababu tunataka wateja watufikie tulipo kitu ambacho hakiwezekaniki. Katika dunia ya sasa, watu wanatakiwa kulifuata soko lilipo. Kati ya bidhaa na mteja, anaanza mteja ndipo inatengenezwa bidhaa kulingana na matakwa ya mteja”.
Alisema kuwa tatizo lililopo ni wajasiriamali kuamua kutengeneza bidhaa baada ya kuona rafiki yake anaitengeneza na kuuza bila kuangalia ukubwa wa soko la bidhaa hizo.
Katika maonesho haya wajasiriamali wamejifunza kile tulichowafundisha darasani na kukiona katika uhalisia wake, aliongeza.
Akiongelea ushiriki wa wajasiriamali katika maonesho ya Nanenane, alisema “huku wamekuja kutangaza bidhaa zao, wamepewa ushauri na kukosolewa juu ya kutengeneza na kuboresha bidhaa zao kutoka kwa watu waliotembelea banda letu, jambo ambalo ni jema katika uboreshaji wa huduma na bidhaa zao”.
Afisa huyo aliwataka wajasiriamali kuacha kulalamika na kuamini katika fedha pekee. Aliwakumbusha kuwa fedha ni kitu cha pili, baada ya kuwa na maono na mawazo sahihi yanayoweza kuwasaidia kutengeneza bidhaa nzuri zinazoweza kushindana na bidhaa nyingine katika soko.
Kuhusu mchango wa SIDO kwa wajasiriamali, Kapinga alisema kuwa, SIDO Mkoa wa Dodoma uliwapatia mafunzo ya kutengeneza bidhaa na jinsi ya kuziingiza sokoni, ushauri wa kibiashara na kuzalisha bidhaa mbalimbali zikiwezo bidhaa za ngozi.
Aidha, SIDO imewakutanisha wajasiriamali na wadau wanaohusika na vifungashio na kupata suluhu ya changamoto ya vifungashio iliyokuwa ikiwakabili wajasiriamali wengi.
Maonesho ya Nanenane mwaka 2020 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Kwa maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, chagua viongozi bora 2020”
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.