Wajumbe wa baraza la wafanyakazi wapitia rasimu ya bajeti 2025/26
Na. Coletha Charles, DODOMA
Baraza la Wafanyakazi Halmashauri ya Jiji la Dodoma limetakiwa kupitia mapendekezo ya rasimu ya makisio ya mpango na bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/26 kwa kutoa mchango wa mawazo kwa lengo la kuboresha nyaraka za bajeti kwa kutengeneza mazingira rafiki kwa wageni na wenyeji wa Mkoa wa Dodoma.
Hayo yalisema na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi pia Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko, katika ukumbi wa mikutano wa halmshauri hilo, alipokuwa akifungua kikao kwa ajili ya kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 pamoja na mpango wa makisio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Alisema kuwa mawazo hayo ni moja ya utekelezaji wa kila mtu kuifanya Dodoma iwe kimbilio la watu wengi duniani kwa kutamani kufika na kuwekeza. “Ninaomba mtoe mawazo yenu tunajua mpo wengi wenye uwezo katika maeneo yenu, tumieni fursa ya kuja kutoa mchango wa nini kifanyike na kwa thamani gani. Miongoni mwa wengi na nyinyi mmebahatika kuwa wajumbe wa baraza hili, sasa tutumie hii bahati na neema ya mwenyezi mungu, kuwafanya nyie kuwa wajumbe muweze kutoa mchango wenu wa dhati ili unapoona Dodoma inabadilika uweze kujivunia kwamba hii ilikuwa sehemu ya mchango wangu” alisema Dkt. Sagamiko.
Mwenyekiti wa baraza hilo, aliongeza kuwa bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26 ni bajeti ya kimkakati zaidi kwa ajili ya kuboresha mazingira na kumaliza miradi vipolo, ambapo mwaka fedha 2026/27, fedha itakayopelekwa kwenye kata inaweza kuongezeka zaidi na kipaumbele kikubwa ni sehemu za kutolea huduma na walengwa ni watumishi wa umma katika kuboreshewa mazigira yao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prosper Kyaruzi, alibainisha kuwa kikao hiko kilikuwa maalum kwa ajili ya kupitisha rasimu ya makadilio ya kujadili bajeti kabla haijaenda kwenye baraza la madiwani kwa ajili ya kupitishwa.
Alisema kuwa baraza hilo lina umuhimu mkubwa kwa wawakilishi wa wafanayakazi kwa kujadili na kuangalia vipaumbele ambavyo vimewekwa na idara moja baada ya nyingine kwa kukubaliana navyo, kufanyiwa kazi na badae bajeti inapitishwa kwa kuangalia mstakabali na masilahi ya wafanyakazi. “Kwanza tumempokea mkurugenzi mpya kwenye kikao cha kwanza cha baraza la wafanyakazi, Dkt. Frederick Sagamiko, amekuwa na sisi kuanzia mwanzo wa kikao hadi mwisho. Nimefurahi sana kwa upande wa sisi walimu tunaowakilisha idara ya msingi na sekondari amesema tutakuwa na kikao kwa ajili ya kujadili stahiki mbalimbali za walimu ambazo zilikuwa bado hazijatimizwa. Lakini pia tumeona tuna Mkurugenzi mwajibikaji ambaye anaupendo mkubwa sana” alisema Kyaruzi.
Ikumbukwe kuwa, kwa mwaka wa fedha 2023/24 Halmshauri ya Jiji la Dodoma ilikadiria kutumia jumla ya shilingi bilioni 123.8 kutokana na vyanzo mbalimbali vya mapato, mwaka wa fedha 2024/25 Halmshauri hiyo ilikadiria kutumia jumla ya shilingi bilioni 143.1 kutokana na vyanzo mbalimbali vya mapato na rasimu ya makisio ya mpango na bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/26 ni jumla ya shilingi bilioni 147.9 kati ya fedha hizo shilingi bilioni 67.3 ni mapato ya ndani, ruzuku ya mishahara shilingi bilioni 65.7, ruzuku ya miradi ya maendeleo shilingi bilioni 11.7 na ruzuku ya matumizi mengineyo shilingi bilioni 3.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.