WAKALA wa Misitu Tanzania (TFS) wilaya ya Morogoro unakusudia kukusanya kiasi cha Sh milioni 433 kwa mwaka wa fedha 2020/2021 kutokana na tozo za mazao ya misitu ( Forest Royalty) .
Kufuatia tozo hizo , halmashauri ya wilaya ya Morogoro itajipatia asilimia tano na mapato yatakayokusanywa na wakala huo halmashauri hiyo pia itapata fedha za ushuru wa miti pandwa (tozo za mbao).
Kaimu Meneja wa TFS, wilaya ya Morogoro, John Kimario alisema hayo jana katika taarifa yake kwa mkuu wa wilaya ya Morogoro, Bakari Msulwa kabla ya kufungua kikao cha uvunaji wa mazao ya misitu kwenye wilaya hiyo.
Kimario alisema kutokana na changamoto za uvunaji na biashara ya mazao ya misitu, serikali mwaka 2007 iliandaa mwongozo wa uvunaji kwa kuwashirikisha wadau wa misitu na kutolewa mwongozo wa uvunaji endelevu wa kibiashara ya mazao ya misitu yanayovunwa kwenye misitu ya asili.
Alisema madhumuni ya mwongozo huo ni kuhakikisha yanakuwepo matumizi endelevu ya rasilimali za misitu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.
Kimario alisema serikali iliunda chombo cha kusimamia uvunaji wa mazao hayo katika kila wilaya na kuwa na kamati ya wilaya ya kusimamia uvunaji wa mazao ya misitu kwa kuzingatia mpango wa uvunaji wa wilaya ulioandaliwa na Wakala huo ngazi ya wilaya.
Alisema uvunaji wa miti ya asili katika maeneo ya msitu wa mataji ( General Lands) utafanyika katika vijiji vya Seregete A na B , Mkulazi , Kidunda , Nyarutanga , Dakawa , Sesenga na Lumbachini .
Kaimu Meneja wa TFS Wilaya hiyo alisema vijiji hivyo nane vinafuata mpango wa uvunaji wa wilaya ambao umeandaliwa na kusimamiwa na wataalamu wa Misitu.
Hata hivyo ,alisema uvunaji katika maeneo ya vijiji kwa miti ya asili ,utavunwa vijiji vinne ambavyo ni Mlilingwa, Matuli , Diguzi na Lulongwe ambavyo vinafuata mpango wa uvunaji wa vijiji na fedha zinazokusanywa na serikali ya kijiji husika na ushuru kwa halmashauri ya wilaya.
Alisema pia kijiji cha Lulongwe hakitakuwemo katika mpango huo kutokana na kutokidhi vigezo vinavyohitajika. Katika hotuba ya ufunguzi wa kikao hicho Mkuu wa wilaya hiyo, Msulwa alisema wilaya ya Morogoro inakabiliwa na tatizo kubwa la uharibifu wa misitu kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu.
Alizitaja baadhi ya shughuli hizo kuwa ni ukataji miti kwa ajili ya kupata nishati , kilimo cha kuhamahama , uchomaji mkaa, upasuaji mbao na ufugaji.
Mkuu huyo wa wilaya alisema moja ya matokeo ya shughuli hizo ni uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji unaosababisha upungufu mkubwa wa maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu, kilimo, mifugo na viwanda.
Chanzo: HabariLeo
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.