Wakala wa umeme vijijini kufikia vitongokji 15 Mkoa wa Dodoma
Imewekwa tarehe: October 18th, 2024
Wakala wa Usambazaji Nishati ya Umeme Vijijini (REA) Mkoa wa Dodoma, leo Oktoba 18, 2024 wamemtambulisha Mkandarasi mpya ambaye ni Kampuni ya Kitanzania ya DERM GROUP itakayoshughulika na mpango wa usambazaji umeme kwenye vitongoji 15 vya kila jimbo la Mkoa wa Dodoma.
Akizungumza wakati wa utambulisho huo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary S. Senyamule amesema, kupitia mpango huo, Mkoa unakwenda kupata vitongoji zaidi vitakavyofikiwa na huduma ya umeme.
“Mkoa wa Dodoma una majimbo 10, kupitia mpango huo, vitongoji vipya 150 ambavyo havikua na umeme vinakwenda kufikishiwa umeme. Mpaka sasa vitongoji vinavyohudumiwa na REA vyenye umeme ni 1631 lakini ukiongeza 150, Mkoa utakua na jumla ya vitongoji 1781 vilivyofikiwa na umeme.” Mhe. Senyamule.
Aidha, Msimamizi wa REA Kanda ya kati Bi. Anneth Malingumu, amesema mradi huo ambao utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 18.5 unatarajiwa kunufaisha kaya 4900 pindi utakapokamilika na ametoa rai kwa wananchi kutunza miundombinu yake ili kuepusha gharama za ziada za matengenezo.
Naye, mwakilishi wa Kampuni ya DERM GROUP Bi. Khadija Mukiza, amesema kampuni yake imejipanga kuifanya kazi kwa ufanisi mkubwa kwani mpaka sasa wameshamaliza kufanya usanifu kwenye vitongoji vyote vya mradi. Zoezi linaloendelea ni kupeleka nguzo, na wameingia mkataba wa miezi 24.