WANANCHI 8570 wakazi wa Kata ya Mkonze katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma wananufaika na huduma ya maji safi ya bomba kufuatia kukamilika kwa mradi wa Maji katika Kata hiyo ulitekelezwa na Manispaa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi iliyowasilishwa kweye Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), mradi huo uliotekelezwa chini ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji awamu ya kwanza, ulianza kujengwa Septemba, 2012 na kukamilika Machi, 2014 kwa gharama ya Shilingi 497,263,970 ukiwa na vituo 15 vya kutolea maji.
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ilitembelea mradi huo jana na kuishauri Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kuharakisha taratibu za kukabidhi mradi huo kwa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dodoma (DUWASA) ambayo kwa mujibu wa sheria ndiyo yenye dhamana ya kutoa huduma ya Maji mjini.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mheshimiwa Vedasto Ngombale aliwaogoza wajumbe wa Kamati yake katika ziara ya kukagua ufanisi wa mradi huo.
Akizungumza kwa niaba ya Kamati katika eneo la mradi, Mheshimiwa Ngombale ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Kilwa Kaskazini, alisema ni muhimu mradi huo kuwa chini ya DUWASA kwani umeshakamilika na uko eneo la mjini, badala ya kuwa chini ya Manispaa na kusimamiwa na Jumuiya ya Watumiaji Maji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi aliahidi kutekeleza ushauri na maelekezo yote ya Kamati hiyo kwa wakati ili malengo ya Serikali ya kusogeza huduma muhimu karibu na wananchi yakamilike.
Tayari Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma iko katika hatua za mwisho za kukakabidhi mradi mwingine wa maji kwa DUWASA uliotekelezwa katika Kata ya Ng’hong’ona ukiwa katika hatua ya mwisho ya ukamilishwaji ambapo wananchi 8318 watanufaika na mradi huo wenye vituo 20 vya kutolea maji.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.