Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WAKAZI wa Kata ya Mkonze iliyopo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kujitokeza kushiriki katika mazoezi ya usafi wa mazingira siku ya Jumamosi ili kuyaweka maeneo yao safi na kuepukana na magonjwa yanayosababishwa na uchafu.
Wito huo ulitolewa na Mlezi wa Kata ya Mkonze, Gratian Mwesiga alipofanya ziara ya kukagua hali ya usafi katika mitaa ya kata hiyo mapema leo.
Mwegasi ambae pia ni Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi Jiji la Dodoma alisema kuwa zoezi la usafi katika Kata ya Mkonze halikufanyika kwa kiwango cha kuridhisha.
“Ni kweli tumetembelea baadhi ya mitaa na kukuta maeneo hayajafanyiwa usafi na baadhi ya maeneo ya biashara kufunguliwa. Leo nimelazimika kutoa elimu kwa wananchi. Nimetoa elimu juu ya umuhimu wa usafi wa mazingira mita tano kuzunguka maeneo ya makazi na biashara. Kwa yale maeneo ya biashara ambayo yalikuwa yakiendelea na biashara wakati nakagua saa moja asubuhi, nililazimika pia kukagua leseni zao. Katika ukaguzi huo nimebaini kuwa baadhi hawana leseni na wengine leseni zimeisha muda wake. Nimewaagiza kukata leseni za biashara” alisema Mwesiga.
Alisema kuwa siku ya Jumamosi ni muhimu kwa kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma. Alisema kuwa usafi ni tabia ya kistaarabu. “Wananchi hawatakiwi kupuuzia suala la usafi wa mazingira kwa sababu usafi unatuepusha na magonjwa yanayosababishwa na uchafu. Wananchi wanatakiwa kukumbuka kuwa Dodoma ni makao makuu ya nchi, hatuwezi kuwa na makao makuu ambayo uchafu ni sehemu ya maisha” alisema Mwesiga.
Aidha, alihaidi kufanya kikao na viongozi wa Kata na Mitaa ili kukubaliana mikakati ya kufanya usafi na ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Kwa upande wake mkazi wa Muungano, Yonas Misana alisema kuwa uongozi wa mtaa umekuwa na utaratibu wa kuwataarifu eneo la kufanya usafi wa pamoja ila wiki hii hawakutaarifiwa ndiyo sababu wakaamua kuendelea na biashara zao.
Mlezi wa Kata ya Mkonze Gratian Mwegasi (kulia) ambae pia ni Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma akimhimiza mmoja wa wakazi wa Mkonze kuhusu kufanya usafi kwenye maeneo yanayozunguka biashara, makazi na taasisi leo wakati alipotembelea kata hiyo kukagua shughuli za usafi.
Mfanyabiashara wa kata ya Mkonze aliyekutwa na mpiga picha wetu akifanya usafi kuzunguka eneo la biashara yake kwa hiyari ili kuweka mazingira safi kwa biashara na afya ya wateja.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.