WAKAZI wa Mkoa wa Dodoma na Mikoa ya jirani wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika maonyesho ya Jeshi la kujenga Taifa (JKT) yanayoendelea katika viwanja vya Jengo la SUMA JKT Medeli Mashariki ikiwa ni wiki ya maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwake.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule leo Julai 4, 2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Jengo la Mkapa Jijini Dodoma.
Mhe. Senyamule amesema kuwa Maonyesho hayo yameanza Julai 1 hadi 9 ndio itakuwa ni kilele chake na yanatarajiwa kufanyika katika viwanja vya Jamhuri Mkoani Dodoma.
"Niko hapa kutoa rai kwa wakazi wa Dodoma na watanzania wa mikoa ya jirani kutenga muda wao kutembelea maonesho hayo kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali yaliyofanywa na Jeshi letu”, amesisitiza Mhe. Senyamule
Vile vile amesema katika maonyesho hayo kuna teknolojia mbalimbali kuhusu masuala ya kilimo, uvuvi, useremala na kadha wa kadha.
Aidha, Mhe. Senyamule ametoa wito kwa vijana kujitokeza kwa wingi kushiriki maonyesho hayo ili kupata fursa mbalimbali zilizopo katika maonyesho hayo.
"Ni fursa kubwa sana kwa jamii hususan vijana kutembelea eneo hilo la maonesho kwa lengo la kujifunza namna ya kujiajiri kwa kutumia fursa zilizopo hapa nchini" amebainisha Mhe. Senyamule
Hata hivyo, ameendelea kutoa wito kwa wananchi wote kwa ujumla wa Mkoa huo kujitokeza kwa wingi siku ya kilele ya maadhimisho hayo katika Viwanja vya Jamhuri na kusisitiza kuwa viwanja vitakuwa wazi kuanzia saa 12 asubuhi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.