WAKAZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kujipanga kwa ufugaji ng’ombe wa kisasa ili waweze kuwahudumia ng’ombe wao vizuri na kupata maziwa mengi.
Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Gratian Mwesiga (pichani juu) alipokuwa akiongea na waandishi wa habari waliotembelea banda ya mifugo katika maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika eneo la Nzuguji jijini hapa.
Mwesiga alisema kuwa katika maonesho ya Nanenane mwaka 2020, Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeleta teknolojia rahisi ya ufugaji wa kisasa unaozingatia masharti ya kitaalam kwa lengo la kumpatia tija mfugaji.
Alisema “ufugaji wa kisasa ni ufugaji unaozingatia utunzaji wa ng’ombe, ulishaji wa ng’ombe, matibabu ya ng’ombe, kalenda ya chanjo kwa ng’ombe izingatiwe, ng’ombe apewe chakula kulingana na uzito wake na kuzingatia ulaji wa chakula cha ziada kama mashudu”.
Wananchi wenye dhamira ya kufuga wanaotembelea banda la Halmashauri ya Jiji wanafundishwa matumizi ya teknolojia na kushauriwa kuzingatia ufugaji wa kisasa wa ndani (zero grazing) ambao unatija zaidi. “Ng’ombe akisafiri umbali mrefu nguvu za kuzalisha maziwa zinapungua sababu chakula badala ya kutumika kuzalisha maziwa kinakuwa kikitumika kwa kutembea huku na kule. Hapa tunatoa elimu ili ng’ombe waweze kutoa maziwa kuanzia lita 15-20. Tunataka tutoke kwenye ufugaji wa asili ambao ng’ombe mmoja anatoa lita 2, huu ni ufugaji ambao hauna tija” alisema Mwesiga.
Akiongelea changamoto ya malisho ya ng’ombe, Afisa Mifugo huyo alisema kuwa katika banda lao elimu ya ulimaji na utunzaji wa malisho inatolewa. “Tuna shamba darasa kwa ajili ya malisho ya mifugo, yapo malisho yanayotokana na mikunde, malisho yanayotokana na nyasi. Nichukue nafasi hii kuwakaribisha wananchi wote wenye nia ya kufuga waje katika banda la mifugo na uvuvi kujionea teknolojia hizo na njia rahisi ya kupanda malisho na utunzaji wake” alisema Mwesiga.
Maonesho ya Nanenane mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Chagua Viongozi bora 2020”
Ng'ombe wakihudumiwa katika banda kwenye maonesho ya Nanenane kutoka kwa wataalam wa Mifugo wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.