Na Getruda Shomi, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imetoa wito kwa wakazi wa Jiji hilo kutumia fursa zinazotokana na uwepo wa taka ngumu ikiwemo kujiajiri kutokana na uuzaji na ununuaji wa taka hizo zinazoweza kurejerezwa kwenye viwanda na kujipatia kipato.
Wito huo umetolewa na Afisa Mazingira katika Halmashauri hiyo Ally Mfinanga (mwenye mic pichani juu) alipotembelea shule mbalimbali za msingi na sekondari ili kufikisha elimu ya utengaji wa taka ili kuweza kuzitumia kwa matumizi mengine kama kutengeneza gesi, kuzirejeleza viwandani na kutengeneza mbolea.
Alisema kuwa taka zinaweza kutumika katika sehemu tofauti ambazo zinaweza kuleta manufaa katika jamii.
“Taka ni fursa kubwa ya kiuchumi, zinatengenezea watu kipato na sisi kama Halmashauri tunanunua taka zinazorejelezwa lakini pia tumesajili makampuni mengi yanayokusanya taka na yanazinunua, hivyo watu wanapata kipato” alisema Mfinanga.
Akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kiwanja cha Ndege, Mfinanga aliwaambia wanafunzi hao kuwa, taka zina manufaa mengi katika jamii hivyo wasichome ila wazitenganishe katika vyombo tofauti zile zinazooza na zisizooza ili waziuze kwenye makampuni yaliyojikita katika ununuzi wa taka hizo.
“Mnapokuwa nyumbani na maeneo mengine mzitenganishe taka ili tuweze kuzirejeleza viwandani pamoja na matumizi mengine kama kutengenezea gesi ambayo itatumika kama nishati, waelezeni na kuwaelimisha wazazi na walezi namna ya kutenganisha taka kama ambavyo tumefundishana hapa leo” alisema Mfinanga wakati alipotoa elimu ya kutenganisha taka na fursa zake kwa wanafunzi wa shule ya Msingi Mtemi Mazengo.
Kampeni hiyo iliyodumu kwa siku tatu mfululizo iliambatana na ugawaji wa vifaa vya kutenganishia taka yaani ‘dust bin’ katika sehemu zote ambazo kampeni hiyo ilifanyika ikiwemo kwenye masoko, shule, na maeneo mengine yenye watu wengi.
Maafisa wa Jiji la Dodoma wakiwa mbele vyombo vya kuhifadhia taka kwa kuzitenganisha.
Afisa Mazingira katika Halmashauri hiyo Ally Mfinanga (mwenye koti) akitoa elimu ya utengaji wa taka mbele ya wafanyabiashara (hawapo pichani) wa Soko Kuu la Majengo Jijini Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.