Na. Dennis Gondwe, MSALATO
WAKAZI wa Kata ya Msalato wametakiwa kuwajenga watoto kiafya kwa kuwaandalia lishe bora ili kujenga taifa imara lenye uwezo wa kifikra na uchapaji kazi kwa ajili ya kuliletea maendeleo.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Dodoma, Mwl. Neema Majula alipokuwa akiongea wakazi wa Kata ya Msalato kwenye maadhimisho ya kuelekea siku ya wanawake duninia ngazi ya kata yaliyofanyika katika Zahanati ya Msalato iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mwl. Majula alisema “ndugu zangu hali ya lishe ni muhimu sana kwa watoto wetu. Tunapoanza kuwajenga watoto hawa wadogo wawe na lishe bora ndiyo tunajenga kizazi bora cha taifa hili. Tunakuwa tunawekeza kwenye afya na akili za watoto ambao baadae wanapoendelea kukua watakuwa wachapa kazi na wenye uwezo mzuri wa fikra na hivyo, kujiletea maendeleo yao na maendeleo ya taifa letu”.
Akiongelea maadhimisho ya kuelekea kilele cha siku ya wanawake duniani, alisema kuwa yanalenga kumhamasisha mwanamke kuchukua hatua kubwa zaidi ya kimaendeleo kuanzia kisiasa, kijamii hadi kiuchumi.
“Hakuna maendeleo yoyote yatafanyika bila kuwa na afya njema. Tukijenga jamii yenye afya nzuri ndiyo, jamii itaweza kufanya shughuli za maendeleo. Kuanzia kwa watoto wetu ili wasipate udumavu, ili wasipate utapiamlo tukianza kuwanjenga tangu wakiwa wadogo ili wawe na afya njema ndivyo tunajenga kizazi chenye afya njema ambacho kitafanya shughuli za maendeleo” alisema Mwl. Majula.
Lishe ya watoto iende sambamba na lishe ya wababa. “Sasa tujikite kwenye lishe ya watoto wetu, na mimi nipanua kidogo, jamani mpaka lishe ya wababa pia kina mama tufanye. Sisi ndiyo waandaaji wa chakula nyumbani tunahitaji kuanadaa lishe kamili nyumbani, tuweke mchanganyiko wa lishe kamili, wanga, vitamini, protini ukijenga familia ambayo ina afya njema ndiyo itaweza kuwaza mambo ya maendeleo” alisisitiza Mwl. Majula.
Kwa upande wa Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Msalato, Dkt. Abusalami Mpamba alisema kuwa amefurahishwa na ziara hiyo kujionea utekelezaji kwa vitendo zoezi la kuwapikia watoto chakula chenye lishe bora. “Mheshimiwa mgeni rasmi, mtoto ukimlea vizuri akiwa na afya bora ndiyo taifa la kesho. Kwa hiyo, wanawake waliopata elimu leo itaweza kutusaidia kupata watoto bora na watakaosoma vizuri, vichwa vyao vitakuwa na akili nzuri kwa sababu wana afya nzuri. Mimi nikupongeze wewe mgeni rasmi kwa uamizi wako. Umeona tumewaelekeza kwa vitendo jinsi chakula kinavyoandaliwa, umeona na jinsi wanavyopewa na umeshuhudia watoto wanavyokula hii ni faraja sana kwetu” alisema Dkt. Mpamba.
Awali akitoa elimu ya lishe kwa akina mama waliohudhuria kliniki katika zahanati ya msalato Afisa maendeleo ya jamii kata ya msalato, Alfrida Kitandala alisema kuwa lishe bora ni muhimu kwa mtoto kwa sababu inamsaidia kuwa na uwezo mzuri wa kufikiri.
“Kina mama nawahusia juu ya suala la lishe bora, siyo uji tu kwa mtoto bali ni mchanganyiko wa vyakula vingi, kuna matunda, kuna madini na vitamini ambazo ni mboga za majini. Suala la maji ni muhimu kwa watoto wetu, lakini pia kuna vyakula vya mafuta kama karanga na mafuta tunayotumia. Hivyo, tujitahidi sana kuzingatia lishe kwa watoto wetu ili iwasaidie hata kufikiria kwao shuleni na katika maisha ya kawaida” alisema Chitandala.
Nae mzazi, Jailes Felix alishukuru kwa elimu waliyopewa juu ya lishe kwa watoto. “Nilikuwa namtania Afisa Afya wa kata kwamba zoezi hili ziwe endelevu lituhamasishe tuwe tunakuja kliniki mara kwa mara, maana kina mama wengine kuja kliniki huwa ni nadra sana. Hivyo, Mungu azidi kuwabariki nina hakika tumeelewa sana kile tulichofundishwa leo na tunakwedna kufanyia kazi” alisema Felix.
Maadhimisho ya siku ya wanawake Kata ya Msalato yalifanyika kwa kutoa elimu ya lishe bora kwa wanawake na hamasa ya kujishughulisha yakifanyika katika Zahanati ya Msalato inayozungukwa na mitaa sita ikikadiriwa kuhudumia watu 11,000.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.