WAKUFUNZI wa mikoa nchini ambao ni wataalamu wa Afya kutoka katika hospitali ya Taifa, hospitali za kanda, hospitali maalumu na hospitali za rufaa za Mikoa wamepatiwa mafunzo ya kujikinga na Ebola.
Mratibu wa Mafunzo hayo Dkt. Erick Richard amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwatayarisha wakufunzi hao kukabiliana na Ebola na wanaporudi kwenye Mikoa yao kwenda kutoa elimu hiyo kwa watoa huduma ya afya.
"Wakufunzi hawa tumewafundisha jinsi ya kutambua, kutibu pamoja na kuweza kutumia afua mbalimbali za kujikinga ili waweze kumhudumia mgonjwa wa Ebola pindi anapogundulika bila ya wao kupata maambukizi." Amesema Dkt. Richard.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) wameleta wataalamu wa magonjwa ya Milipuko kutoka nchi ambazo zilishawahi kutokea kwa mlipuko wa Ebola ikiwemo nchi ya Congo DRC, Zambia, Bukinafaso, Cameron na Sierra-Leone kuja kutoa mafunzo hayo nchini.
"Ugonjwa huu hadi sasa haujaingia nchini lakini tumejiandaa na mafunzo haya kuwa ni sehemu ya utayari katika kujijengea uelewa kwa kuujua ugonjwa wa Ebola na kuutibu, kujikinga na maambukizi na kuzuia maambukizi hayo yasisambae." Amesema Dkt. Richard.
Miongoni mwa mambo waliyofundishwa ni pamoja na kuvaa na kuvua vifaa kinga vya kujikinga na Ebola kwa wahudumu, kupata uelewa wa ugonjwa wa Ebola, Jinsi ya kunawa mikono kwa usahihi, mafunzo kwa vitendo namna ya kumpokea mgonjwa wa Ebola na kumhudumia.
Mafunzo hayo yamemalizika kutolewa kwa Mikoa yote 28 Tanzania Bara.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.