Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WAKULIMA na wafugaji wa mikoa ya Dodoma na Singida wametakiwa kuwa wepesi kuwatafuta wataalam ili watatuliwe changamoto zinazowakabili katika kuleta tija kwenye shughuli zao.
Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Dkt. Khamis Mkanachi alipokuwa akifanya majumuisho ya ziara ya kutembelea mabanda ya maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Dkt. Mkanachi alisema “wito wangu kwa wakulima na wafugaji hawajawa wepesi kutoka kuwafuata wataalam wa kilimo na mifugo ili wawatatulie changamoto zao. Mtazamo huu lazima tuubadilishe, wakulima na wafugaji lazima watoke kuwatafuta wataalam ili kuleta tija katika mazao ya kilimo na mifugo”.
Mgeni rasmi huyo alionesha kuridhishwa na maandalizi ya maonesho ya Nanenane mwaka 2022. Mkanachi alisema kuwa maonesho ni mazuri na mazao yanaonekana kuhudumiwa vizuri. “Ndugu zangu, changamoto iliyopo ni ukitoka ukaenda pembezoni kidogo hali ni tofauti. Tuliyoyaona hapa kwenye maonesho yanaweza kuleta mapinduzi makubwa ya kilimo. Pembejeo tulizoziona kwenye maeneo zionekane kwa wananchi” alisisitiza Dkt. Mkanachi.
Akiongelea Sensa ya watu na makazi, Mkuu huyo wa Wilaya ya Kondoa alisema kuwa waandishi wa habari wanatakiwa kuwa vipaza sauti kuelezea umuhimu wa Sensa ya watu na makazi. “Tarehe 23 Agosti, itafanyika Sensa ya sita ya watu na makazi. Waandishi wa habari muwe vipaza sauti ili wananchi wahamasike kuhesabiwa. Sensa hiyo ni ya kihistoria na itakuwa ni Sensa ya sita kufanyika nchini” alisema Dkt. Mkanachi.
Mwananchi aliyetembelea maonesho ya shughuli za wakulima na wafugaji katika viwanja vya Nzuguni, Mwanaisha Juma alisema kuwa yupo tayari kuhesabiwa. “Kuhesabiwa kwani ni nini hadi nisiwe tayari. Kila siku wakubwa wetu tunawaona wakielezea umuhimu wa Sensa ya watu na makazi, lazima nihesabiwe. Nawashauri na watu wengine wote kuhesabiwa ili kuisaidia serikali kufikia kile inachotaka” alisema Mwanaisha.
Maonesho ya shughuli za kilimo na mifugo mwaka 2022 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Agenda 10/30: kilimo ni biashara, shiriki kuhesabiwa kwa mipango bora ya kilimo, mifugo na uvuvi”.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.