WAKULIMA zaidi ya milioni moja kunufaika na mpango wa ukopeshaji wa pembejeo sambamba na upatikanaji wa masoko ya mazao yao kupitia programu ya AFRICA-CONNECT ambayo inaratiiviiwa kwa pamoja na Kampuni ya Mbolea ya YARA, Benki ya EQUIT, Wakala wa Mbegu (ASA), Kampuni ya Viuatilifu CORTEVA na Kampuni ya MURZAH WILMER RICE MILLERS.
Hayo yamesemwa jana Mei 20, 2022 Jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa program ya AFRICA-CONNECT ambapo wakulima watanufaika na mkopo wa mbegu bora, mbolea na viuatilifu pamoja na kupata huduma ya ugani na mwisho wa siku kupata soko la mazao yao. Program hii itaanza kwa wakulima wa mpunga 100,000 kwa mwaka huu ambapo mpunga wao wote utanunuliwa na Kampuni ya Murzah Wilmar.
Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde amewapongeza kampuni ya YARA na wadau wote washirika kwa kuja na mpango wa kusaidia kukuza sekta ya kilimo nchini yenye ajenda mahsusi ya AJENDA 10/30 yenye azma ya kuikuza sekta ya kilimo kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2030 na kuahidi kwa niaba ya serikali kusaidia utekelezaji wa program hii yenye lengo la kumpunguzia mzigo mkulima katika upatikanaji wa pembejeo kwa wakati na kwa uhakika.
“Nawapongeza sana YARA, Equity Bank, Corteva, ASA na Kampuni ya Murzah Wilmar kwa kuja na mpango mzuri wa kumsaidia mkulima wa mpunga kuongeza uzalishaji na kumpunguzia mzigo wa pembejeo.
Hatua hii itasaidia kutoa mchango mkubwa katika kuikuza sekta ya kilimo nchini, wote ni mashahidi na mmeona dhamira njema ya Rais wetu mpendwa Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kuiendeleza na kuikuza sekta ya kilimo ambapo bajeti ya wizara ya kilimo imepanda kutoka shilingi bilioni 294 mpaka shilingi bilioni 751.
Serikali imejipanga kuhakikisha mkulima ananufaika na kamwe haitashirikiana na mdau au taasisi yeyote ambayo itaonesha dalili za kudhulumu au kuwanyonya wakulima.
Kabla ya kuja kushirikiana nanyi kwenye uzinduzi wa program hii nilitumia muda wangu kujiridhisha kma suala hili lina maslahi kwa wakulima” alisema Mavunde.
Aidha, Mhe. Mavunde alishauri na kuzitaka kampuni zote zinazoshirikiana kwenye program hiyo ambayo inalenga kuwazewezesha wakulima wa mpunga kuanza uzalishaji hadi kutafuta masoko, kuongeza wigo na kuwafikia wakulima wa mazao mengine kama mahindi ili kukuza sekta ya kilimo na kuinua uchumi wa wakulima.
Vilevile, Mhe. Mavunde alibainisha kuwa Serikali imeweka mkazo mkubwa kwenye utafiti na uzalishaji wa mbegu bora ili nchi ijitosheleze kwa mbegu na ziada iuzwe nje ya nchi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.