WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Ummy Mwalimu amesema Wakurugenzi wa Halmashauri nchini watapimwa kwa kigezo cha ukusanyaji wa mapato ya ndani katika Halmashauri zao na kutenga fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo inayotatua kero za wananchi.
Akifungua Mafunzo ya Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa jijini Dodoma Waziri Ummy amesema mkakati uliopo ni kuhakikisha Halmashauri zinajitegemea kibajeti na hili litawezekana tu kwa ukukusanyaji wa mapato ya ndani hivyo amewaagiza kukusanya kikamilifu mapato ya ndani katika Halmashauri zao ili kufikia azma hiyo.
Akifafanua zaidi Waziri Ummy amesema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22 ya Mamlaka za Serikali za Mitaa ilijiwekea lengo la kukusanya kiasi cha shilingi Bilioni 863.8 hivyo kila mwezi zinatakiwa kukusanywa shilingi Bilioni 71 na kuanzia Julai hadi Septemba, 2021 zimekusanywa shilingi Bilioni 118 badala shilingi Bilioni 142 hivyo bado ukusanyaji wa mapato upo chini.
Waziri Ummy amesema Mamlaka za Serikali za Mitaa mpaka sasa zilitakiwa ziwe zimekusanya mapato ya ndani kwa asilimia 16 lakini kuanzia Julai hadi Septemba, 2021 makusanyo ni asilimia 14, hivyo amewaagiza kusimamia ukusanyaji wa mapato ili kufikia lengo lililowekwa na Serikali.
Amewataka Wakurugenzi hao kubuni vyanzo vipya vya mapato ambavyo havileti kero wala kudhalilisha wananchi lakini wakihakikisha wanabuni vyanzo vipya vya mapato na kusimamia kikamilifu na kuhakikisha Serikali inafikia malengo yanayokusudiwa.
Aidha, amewata kuhakikisha mapato yanayokusanywa yanaingizwa benki kwa wakati ndani ya masaa 24 na kutumia mfumo wa Kielektroniki wa kukusanyia mapato (LGRCIS) katika suala zima la ukusanyaji wa mapato.
Waziri Ummy amewataka Wakurugenzi hao kuhakikisha kuwa wanatenga asilimia 40 ya mapato ya ndani kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa Halmashauri ambazo zinapata mapato chini ya Bilioni tano na wale wanaokusanya zaidi ya Bilioni tano wanatakiwa kutenga asilimia 60.
"Sitegemei kuona fedha hizi zinatumika kwa ajili ya matumizi ya ofisi, nategemea fedha hizi zijenge zahanati, madarasa, mabweni, maabara, barabara, masoko, stendi na si kugharamia posho za vikao" amesisitiza Waziri Ummy.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.