Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo (Mb) amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanasimamia kwa weledi fedha zilizotengwa kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Waziri ameyasema hayo leo wakati akifungua semina ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakurugenzi wa Halmashauri na Wasimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa iliyofanyika katika Ukumbi wa Auditoriumn, Chuo Kikuu cha Dodoma.
Mhe. Jafo amesema kuwa hatasita kuwachukulia hatua Wakurugenzi ambao wataenda kinyume na utaratibu wa matumizi ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kiuika miongozo iliyotolewa na Serikali katika matumizi sahihi ya fedha hizo.
Aidha, ameonya matumizi yasiyofaa kwa fedha zilizotengwa na kusisitiza kuwa fedha hizo ni za moto, hivyo matumizi yake yanahitaji kufuata miongozo na taratibu zilizowekwa na Serikali.
Ameendelea kusema kuwa ni marufuku kwa Mkurugenzi kutumia fedha za uchaguzi kinyume na agenda ya uchaguzi na kusisitiza haja ya fedha hizo kutumika kwa wakati.
“Naomba niwape tahadhari, katika matumizi ya fedha ya uchaguzi, fedha hizi za uchaguzi zinazokuja ni kwa ajili ya uchaguzi, naomba mtu asidanganyike wala kurubunika kwa lolote katika mchakato huu wa uchaguzi, katika fedha za moto hizi fedha za moto” amekazia Mhe. Jafo.
Waziri amesema kuwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inasimamia kwa karibu Uchaguzi huu, hivyo ni matumaini yake kuwa matumizi ya fedha za uchaguzi yataenda kama ilivyokusudiwa kwa kufuata miongozo ya matumzi ya fedha hizo.
Amewakumbusha Wakurugenzi wote wa Halmashauri nchini kuwa ndio wenye dhamana ya kusimamia matumizi sahihi ya fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kinyume na hapo wanapaswa kujibu hoja zitakazojitokeza za kushindwa kusimamia fedha hizo vizuri.
Kuhusu wasimamizi wa uchaguzi, Mhe. Jafo amewasihi kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuhakikisha ratiba ya uchaguzi inafuatwa huku akiwataka kutambua kuwa wamebeba dhamana kubwa katika kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa kuzingatia Demokrasia.
“Natamani sana mlioteuliwa kuwa wasimamizi wa uchaguzi mwende vizuri mpaka mmalize vizuri kwa mujibu wa kanuni zetu. Mheshimiwa Rais anatamani nchi yake ikatekeleze demokrasia vizuri na ndio maana mnaona ameweza kuwezesha kila eneo kwa lengo kuwa uchaguzi uende ukafanyike vizuri”. Amesema Mhe. Jafo
Amesema Uchaguzi wa Serikali za Mitaa nchini ni muhimu kwa kuwa maisha ya watu yanaanzia katika vitongoji, mitaa na vijiji vyenu, mustakabali wa kuchakata maendeleo lazima uanze katika ngazi husika ambayo uchaguzi huu unaenda kuwapata viongozi na hawawezi kupatikana kama wasimamizi wa uchaguzi mtashindwa kufanya kazi yenu vizuri.
Wakati huohuo, Mhe Jafo amewataka Makatibu Tawala wa Mikoa ambao ndio waratibu wakuu wa uchaguzi kuhakikisha wanafuatilia kwa karibu kila tukio na kuwataka wasikubali kuharibiwa kazi.
“Makatibu Tawala wa Mikoa wao ni waratibu wakuu wa Uchaguzi katika Halmashauri zao kipindi hiki mna kazi kubwa sana ya kuhakikisha huko chini mambo yanaenda vizuri na wala msikubali hata kidogo mtu awaahiribie kazi”. Amesisitiza Mhe. Jafo
Awali, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Joseph Nyamhanga, alieleza kuwa kikao hicho kinalenga kukumbushana majukumu ya uchaguzi huo na kuna matukio mbalimbali yaliyopo katika tangazo la uchaguzi yanayopaswa kutekelezwa.
Mhandisi Nyamhanga amesema OR-TAMISEMI imeshakamilisha maandalizi yote muhimu ya uchaguzi huo na nyaraka mbalimbali zimeandaliwa na kusambazwa ikiwemo kanuni na muongozo wa uchaguzi huo.
Amesema tayari OR-TAMISEMI imeratibu upatikanaji wa fedha na tayari zimeshatumwa kwenye Sekretarieti za Mikoa yote na anaamini zimeshatumwa kwenye Halmashauri kwa ajili ya maandalizi.
Aidha, Nyamhanga alisema katika uchaguzi wa mwaka huu inakadiriwa kutakuwa na vituo vya kupigia kura 110,000.
Chanzo: Tovuti ya tamisemi.go.tz
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.