Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WAKURUGENZI wa mamlaka za serikali za mitaa wametakiwa kutenga fedha katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya kununua vifaa vya Tehama kwa ajili ya kuwezesha mfumo wa ufundishaji mubashara unaomuwezesha mwalimu mmoja kufundisha zaidi ya shule mmoja kwa wakati mmoja.
Agizo hilo lilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohammed Mchengerwa alipokuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa majaribio ya ufundishaji mubashara uliofanyika katika Shule ya Sekondari Dodoma.
“Kama nilivyosema, tuna uhaba wa walimu takribani 271,028 nchi nzima. Mnaweza kuona uhaba huu ni mkubwa sana na jitihada za Rais wetu ambae ametupa maono ya kwenda kupunguza uhaba wa walimu na ndio maana tumekuja na mfumo huu wa Tehama wa ufundishaji mubashara. Nichukue fursa hii kuwapongeza walimu wote wa Kibaha Sekondari na Dodoma Sekondari. Nimejionea majaribio na nimeridhika na kwajitihada hizi sasa niwaelekeze wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kwenye bajeti ijayo 2024/2025 wahakikishe wanatenga fedha za kutosha ili tuanze mchakato wa kununua vifaa hivi vya Tehama. Kwa wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa kuhakikisha wanateua shule maalum ambazo zitakuwa nguzo kwaajili ya kusambaza mfumo huu wa Tehama” alisema Mchengerwa.
Aidha, alimuelekeza Katibu Mkuu Tamisemi kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ili kuhakikisha mfumo huo unaenea nchi nzima ifikapi mwezi Desemba, 2025. “Majaribio haya tunaita ufundishaji mubashara ambayo ni moja ya jitihada za serikali ya awamu ya sita kwa kwenda kupunguza uhaba wa walimu katika maeneo yote nchini” alisema Mchengerwa.
Akiongelea changamoto ya uhaba wa walimu, alisema kuwa Tamisemi ililiangalia jambo hilo la uhaba wa walimu katika nyanja mbili na kugundua uhaba wa walimu bado ni mkubwa sana. “Kwakuwa tumekwenda kwenye majaribio ya Tehama na tunajua yatakuwa na changamoto nyingi sana ikiwemo uhaba wa vifaa, lakini hapa kipekee niwapongeze sana kwa wale ambao walijitolea kutoa vifaa mbalimbali kwasababu jitihada hizi za Rais, Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kwamba tunapunguza changamoto ya walimu lakini pia kuongeza ufahamu kwa vijana wetu wanaosoma shule za awali, msingi na sekondari” alisema Mchengerwa.
Kwa upande wa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Dodoma, Faudhia Said alisema kuwa mfumo huo wa ufundishaji ni mzuri kwasababu utakuwa unasaidia katika zile shule ambazo zina upungufu wa walimu na kuongeza ufaulu kote nchini.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.