KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhandisi Joseph Nyamhanga amewataka wakurugenzi wa Halmashauri kuongeza usimamizi katika fedha zinazokusanywa kupitia mfumo wa kielektroniki ili kuondoa kero zinazowakabili wananchi.
Nyamhanga ametoa maelekezo hayo alipokuwa akifungua semina na mkutano mkuu wa wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa wataalamu wa Tanzania na Osaka Japan (TOA) unaofanyika jijini Dodoma.
Amesema wakurugenzi hao wanatakiwa kuongeza usimamizi wa ukusanyaji wa mapato kupitia mifumo ya kidijitali ili kusaidia kuongeza mapato ya ndani.
“Msimamie hizi fedha ili zileta tija katika kuboresha maeneo mbalimbali ya nchi ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakikabiliwa na changamoto nyingi za huduma kama afya, maji pamoja na elimu,” alisema Nyamhanga.
Aidha, amewataka wakurugenzi hao kuhakikisha wanasimamia kwa karibu fedha zinazotolewa na serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ili ikamilike kwa wakati.
“Moja ya changamoto kubwa ni miradi kutokamilika kwa wakati hali ambayo inachangia hata Wizara ya Fedha kusimamisha baadhi ya miradi ambayo inachelewa kukamilika kutokana na kuongezeka kwa gharama za utekelezaji,” alisema.
Amesema katika eneo hilo wakurugenzi wengi wameshindwa kutimiza wajibu wao, hali ambayo imesababisha wengi wao kusimamishwa, kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na wengine kuondolewa nyadhifa zao.
Pia Nyamhanga amesema bado baadhi ya wakurugenzi wanashindwa kufanya matumizi ya mfumo wa 'Force Account'.
Aliwakumbusha wakurugenzi kuwa wanatakiwa kutumia mwongozo mpya uliotolewa na Tamisemi, unaoelekeza matumizi sahihi ya utaratibu huo.
“Hivi sasa katika utaratibu wa force account kumekuwapo na changamoto ya vifaa kununuliwa kwa bei ya juu, lakini upendeleo kwa hawa mafundi tunaowatumia,” alisema Mhandisi Nyamhanga.
Vilevile amewasisitiza wakurugenzi wote kuhakikisha kuwa wanakamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kuondoa msongamano ulipo katika shule mbalimbali.
“Tuhakikishe kuwa tunakamilisha vyumba vya madarasa katika muda uliopangwa ili kuondoa changamoto ya msongamao kwa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika mwaka wa masomo 2020,” alisema.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wanachama wa TOA, Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Rehema Madenge, alisema watahakikisha wanaitumia jumuiya hiyo kupeleka maendeleo kwa wananchi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.