NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewaelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha Waratibu wa utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wanatekeleza kikamilifu jukumu la kuratibu utekelezaji wa mpango huo ili kuiwezesha Serikali kutekeleza azma yake ya kuzinusuru kaya zote maskini nchini.
Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo wakati wa kikao kazi chake na Waratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wa Halmashauri za Mkoa wa Kilimanjaro ikiwa na lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Waratibu hao mkoani humo.
Naibu Waziri huyo amewataka Wakurugenzi hao kuwapa Waratibu wa TASAF muda wa kutosha wa kutekeleza majukumu yao kikamilifu badala ya kuwabadili kila mara, kitendo kinachosababisha kutokuwa na mwendelezo mzuri wa usimamizi wa miradi ya TASAF nchini.
“Mradi wa TASAF ni mradi mkubwa sana wa kimkakati ambao unagusa moja kwa moja maisha ya mamilioni ya Watanzania wa kipato cha chini, hivyo kukiwa na mabadiliko ya mara kwa mara ya waratibu yataathiri mwendelezo mzuri wa usimamizi wa miradi ya TASAF,” Mhe. Ndejembi amefafanua.
Ameongeza kuwa, TASAF inapeleka fedha nyingi za ruzuku kwa walengwa kwenye miradi ya maendeleo, miradi ya ajira za muda, miradi ya kuboresha sekta ya afya na sekta ya elimu hivyo, Serikali inahitaji kuwa na Waratibu watakaokuwa na muda wa kutosha wa kusimamia vizuri mchakato mzima wa utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani Kilimanjaro, iliyokuwa na lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma ikiwa ni pamoja kusisitiza usimamizi mzuri wa utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini unaoratibiwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.