Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WAFANYABIASHARA katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kufanya shughuli zao kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa kwa kukata leseni za biashara ili kuepuka misuguano na kuchukuliwa hatua kwa kukiuka taratibu zilizopo.
Ushauri huo ulitolewa na Mkuu wa Kitengo cha Usafi na uthibiti wa taka ngumu, katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro alipokuwa akiongelea tathmini ya siku ya kwanza ya utekelezaji wa oparesheni ya kukusanya mapato katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Kimaro alisema kuwa katika oparesheni hiyo iliyofanyika katika Kata ya Ihumwa ilibaini kuwa wafanyabiashara wengi hawana leseni za biashara. “Timu ya Menejimenti iliunda makundi ya wakuu wa divisheni na vitengo kwenda kufuatilia hali halisi ya ukusanyaji mapato. Zaidi ya wafanyabiashara wengi kutokuwa na leseni, tulibaini wengine walilipia leseni zao ila hawajaenda kuzichukua halmashauri. Asilimia kubwa hawajalipa ushuru wa huduma kwa mujibu wa sheria” alisema Kimaro.
Akiongelea hatua zilizochukuliwa, alizitaja kuwa ni kutoa elimu kwa wafanyabiashara hasa ushuru wa huduma. “Baadhi ya maeneo tulilazimika kufunga kutokana na unyeti wake hasa maeneo ya kuuza vilevi ili waweze kukata leseni zao na ushuru wa huduma kwenye maeneo yao” alisema Kimaro.
Oparesheni ya kukusanya mapato ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ni utekelezaji wa tathmini iliyofanywa na timu ya menejimenti ya mwenendo wa makusanyo ya mapato na kutoridhika na mwenendo huo kwa baadhi ya vyanzo vya mapato na kuamua kuingia katika mitaa mbalimbali ya jiji hilo kusaka mapato.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.