WAKUU wa Idara na Vitengo wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wanaanza zoezi la siku 14 la kukagua Mikataba ya wafanyabiashara waliopanga katika Masoko ya Jiji, maeneo ya wazi pamoja na majengo mengine ya Halmashauri ambapo lengo ni kuhakikisha kila anayefanya biashara ana nyaraka halali ikiwemo mkataba wa pango na leseni.
Akiongea mapema leo Machi 13, 2019 kabla ya kuanza kwa zoezi hilo, Kaimu Mkuu wa Idara ya Fedha na Biashara wa Halmashauri hiyo Rahabu Philip amesema kuwa zoezi hilo litahusisha Wakuu wote wa Idara na Vitengo.
“Zoezi hili ni la kawaida na litahusisha Wakuu wa Idara na Wakuu wa Vitengo wote kwa sababu wao ndiyo watoa maamuzi katika jiji letu na wataweza kujua hali halisi ilivyo katika maeneo ya ukusanyaji mapato” Alisema Rahab.
Alisema baada ya kuona hali halisi watajipanga kuona jinsi watakavyosaidia kupanga mipango ya ukusanyaji mapato ya Serikali na kuzuia mianya ya upotevu wa mapato hayo, na kuwa matarajio baada ya zoezi hilo ni kuona kiwango cha ukusanyaji mapato kinaongezeka.
“Hali ya ukusanyaji mapato katika Jiji la Dodoma ni ya kuridhisha, japokuwa kuna baadhi ya maeneo yanayosuasua kidogo ndiyo maana tumekuja na zoezi hili ambalo litaamsha ari ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali ili tuzidi kutoa huduma bora kwa Wakazi wa Jiji letu na Watanzania kwa ujumla” alisema Philip.
Aidha, alitoa wito kwa Wananchi hususani Wakazi wa Jiji la Dodoma kuendelea kulipa kodi kwa hiari kwa ajili ya maendeleo ya jiji hilo na Taifa kwa ujumla.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.