Timu ya Uongozi ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma (CMT) imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Afya Mkonze kwa lengo la kuimarisha afya za wananchi na kujipanga kuhakikisha mipaka ya kituo hicho inawekewa alama.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa timu hiyo ya uongozi ya Halmashauri, Shaban Juma baada ya kutembelea na kukagua ujenzi unaoendelea wa kituo hicho kilichopo katika Kata ya Mkonze.
Juma alisema kuwa hali ya ujenzi huo inaenda vizuri kwa mujibu wa ratiba ya kazi iliyopo. Alisema kuwa matarajio ya timu hiyo ya uongozi ya Halmashauri kuwa ujenzi huo utakamilika ifikapo tarehe 16 Julai, 2019 kwa mujibu wa mpango kazi uliopo.
Juma alisema kuwa maeneo ya mipaka ya kituo hicho cha afya yabainishwe na kuwekewa alama ili kuepuka uvamizi na makazi holela katika eneo la kituo hicho. Utambuzi na uwekaji wa mipaka ya kituo hicho utasaidia kuondoa migogoro na wananchi hasa kituo hicho kitakapohitaji upanuzi.
Maelekezo mengine yaliyotiliwa mkazo ni kuongeza kasi ya utaratibu wa manunuzi ya milango 50 ukamilike na kupachikwa ili kuruhusu taratibu nyingine za ujenzi wa ndani ziweze kuendelea. Vilevile, uongoz wa kituo hicho cha afya ulielekezwa kufanya usafi wa mazingira ili kuboresha mandhari ya kituo hicho.
Awali Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Dkt. Baraka Chaula alisema kuwa serikali ilitoa kiasi cha shilingi milioni 400 kwa ajili ya upanuzi wa kituo cha afya Mkonze kwa maelekezo. Maelekezo hayo aliyataja kuwa ni ujenzi wa jengo la wazazi, jengo la upasuaji, jengo la maabara, jengo la kuhifadhia maiti na nyumba ya mtumishi.
Timu ya Uongozi ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilihamishia kikao chake cha “Morning prayer’ katika miradi ya Kituo cha Afya Mkonze, shule ya msingi ya mfano inayojengwa Ipagala na eneo itakapojengwa shule ya sekondari ya mfano Iyumbu, kwa lengo la kukagua maeneo ya ujenzi huo na kuwa na uelewa wa pamoja juu ya miradi hiyo mitatu.
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mkonze Baraka Chaula akitoa maelezo kuhusu maendeleo ya kazi ya ujenzi kituoni mbele ya Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma
Wakuu wa Idara na Vitengo walipotembelea kuona maendeleo ya upanuzi wa kituo cha Afya Mkonze.
Mwalimu Joseph Mabeyo Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi wa Jiji la Dodoma akitoa maelezo kuhusu mradi, changamoto na mafanikio yaliyofikiwa katika ujenzi wa Shule ya Msingi ya Mfano.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.