KATIKA kupambana na ugonjwa wa Corona Serikali imewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini kuhakikisha wanahimiza maelekezo yaliyotolewa na wataalam wa afya ya kudhibiti maambukizi ya awamu ya tatu ya virusi vya Korona (COVID 19) katika maeneo yao.
Amewataka kuhakikisha wananchi wanavaa barakoa wanapokuwa kwenye mikusanyiko, kufanya mazoezi, kutumia vipukusi mikono, kuzingatia matumizi ya lishe bora na kuhakikisha kunakuwa na maji tiririka kwenye maeneo yote ya mikusanyiko.
Agizo hilo limetolewa leo jijini hapa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima alipofanya ziara yake ya kustukiza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
"Viongozi wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha mnaendelea kutoa elimu kwa wananchi wenu hasa kipindi hiki ambacho wagonjwa wa Covid 19 wameanza kujitokeza ili maambukizi yasiendelee kuenea kwa kasi elimu hiyo itolewe kwa kutumia redio za kijamii na mikutano ya hadhara;
Rais Samia tayari alisema wagonjwa wapo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kibaigwa hivyo wananchi wanatakiwa kulichukulia suala hili kwa ukubwa wake na kuanza kuchukua tahadhari wao wenyewe kwasababu kila mtu anawajibu wa kutunza afya yake,"
Waziri Dkt. Dorothy amesisitiza kuwa wananchi waendelee kutumia tiba asili kwani serikali haijazuia matumizi ya tiba asili kwani imeweza kuisaidia jamii kwenye kudhibiti maambukizi ya Korona katika wimbi la kwanza, la pili hata la tatu pia itasaidia.
"Tusianze kupeana wasiwasi lakini pia ukiona dalili hizo haraka wahi kituo cha afya hiyo ndio vita tunatakiwa kupigana nayo" amesema Gwajima.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma kuhakikisha magari yote ya kubeba abilia hayajazi na hatua kali zichukuliwe kwa madereva watakao kiuka agizo hilo kwa mujibu wa vifungu vya sheria.
"Wamiliki wa magari katika hili mtatuvumilia katika hili tunataka maeneo yote ya magari yanapoanzia safari ya kwenda mikoani na maeneo mengine ndani ya mkoa tuhakikishe watu wamekaa kwenye ‘siti’ atakayekiuka agizo na kusimamisha watu njiani atachukuliwa hatua za kisheria kwasababu hapo tunaokoa maisha ya mtu" amesema Mtaka.
Aidha, katika eneo lingine Mtaka amewataka wafanyabiashara wote katika masoko wahakikishe wanavaa barakoa na katika milango yote ya kuingilia sokoni kuhakikisha kunakuwa na sehemu za kunawia mikono kwa kutumia maji tiririka.
"Katika maeneo ya minadani muhakikishe mnavaa barakoa kwasababu tunaposema suala la uhai wa mtu siyo suala la Serikali anapokufa mtu haifi Serikali wala hospitali, kanisa wala msikiti sisi kama Serikali tunakua tumetimiza wajibu" amesema Mtaka.
Sambamba na hayo pia amewataka Wakuu wa Wilaya zote wahakikishe wanaandaa vipindi kwenye redio za jamii ambazo ni rahisi hata wananchi waishio vijjini wajue namna ya kujikinga na kutoa matangazo kwenye maeneo ya mikusanyiko kuwakumbusha wananchi kuendelea kuchukua tahadhali.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma Mjini, Meja Msataafu Johnick Risasi alisema Covid 19 itadhibitika endapo kila mtu atatekeleza wajibu wake katika eneo lake kwasababu ni gonjwa la mlipuko ambalo litadumu kwa muda mrefu.
"Naishauri Serikali kuendelea kuweka sheria mbalimbali zenye lengo la kudhibiti maambukizi yasienee kwa kasi zikiwemo sheria kwenye Vyombo vya usafiri kutojaza abilia, kuhamasisha wananchi kunawa mikono kila mara itasaidia kuvuka salama katika wimbi hili la tatu," ameeleza.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.