VIONGOZI wa taasisi, mashirika na makampuni 183 kati ya 187 wamenusurika kufukuzwa kazi baada ya kutekeleza agizo la Rais John Pombe Magufuli kwa kufanikiwa kutoa gawio na michango kwa serikali kiasi cha shilingi bilioni 25.12.
Aidha, taasisi nne zimeshindwa kulipa gawio na michango kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kutokuwa na uzalishaji, upya wa taasisi na kampuni nyingine kurejeshwa serikalini kutokana na mwekezaji kutokidhi vigezo vya mkataba wa ubinafsishaji.
Novemba 24, mwaka jana, Rais Magufuli alizitaka taasisi, mashirika na kampuni kuwasilisha gawio na michango ya huduma za jamii ndani ya siku 60 ambazo zilikamilika jana saa sita usiku.
Akizungumza jana katika hafla ya kupokea hundi za gawio na michango, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema agizo la Rais limetekelezwa kwa asilimia 100 na amevunja rekodi kwa kuwa haijawahi kutokea katika historia ya nchi.
"Kwa kweli zoezi hili kwangu halikuwa rahisi sana, nikifikiria uwingi wa idadi ya taasisi, mashirika na kampuni 187 ambazo hazikuwa zimechangia, nilijua kabisa lazima damu ya wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu itanimwagikia, lakini naona hali imekuwa tofauti kabisa," alisema.
Alisema mwenyekiti wa bodi yeyote na mtendaji mkuu husika angekuwa ameonyesha utovu wa nidhamu kwa kukaidi amri ya Rais alikuwa tayari kuwafukuza kazi jana na wangeondoka na aibu kubwa ya kushindwa mbele ya macho ya Watanzania.
"Kila siku huwa naeleza kuwa hii kazi ya Waziri wa Fedha ni ngumu, maana fedha nyingi zinahitajika, na kila sekta ili kutekeleza shughuli mbalimbali za serikali za kupeleka maendeleo kwa wananchi," alisema.
Alisema kuongeza ukusanyaji wa mapato na kulipa gawio na michango ya huduma za jamii kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali ni njia ya uhakika ya kujitegemea na kuondokana na fedheha ya kutegemea kuomba misaada nje ya nchi.
"Natamani awamu hii ikiisha tuwe tumefikia kukusanya Sh. trilioni mbili kwa mwezi, mwaka 2020 msisubiri Rais atoe maelekezo ndipo muanze kulipa gawio na michango," alisema.
Aliwataka viongozi wa taasisi hizo kuwajibika ipasavyo kuinua utendaji na kulipa gawio ili kuisaidia serikali kutekeleza shughuli za maendeleo.
Alisisitiza kupunguza matumizi yasiyo ya lazima katika mashirika na taasisi kwa kuwa si vyema nchi maskini viongozi wa taasisi kutanua.
Naye Msajili wa Hazina, Dk. Athuman Mbuttuka, alisema Rais alipokea gawio na michango kutoka kwa taasisi, mashirika na kampuni 79 kati ya 266 kiasi cha Sh. trilioni 1.05.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.