Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mtaa Mhe. Angellah Kairuki amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa kuhakikisha wanazisimamia halmashauri zote kufunga hoja za ukaguzi wa hesabu za serikali.
Ametoa maagizo hayo leo Novemba 25, 2022 alipokuwa akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Simiyu kabla ya kuanza ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani humo.
"Kuna Halmashauri wana hoja ambazo zipo kwa muda wa miaka miwili hadi mitatu kutokana labda na uzembe wa kutoambatanisha nyaraka, hakikisheni mnazisimamia halmashauri hizo ili zijibu hoja kwa wakati na kuzifuta kabisa," amesisitiza Waziri Kairuki.
Ameziagiza Halmashauri kuhakikisha hoja hazijirudi na elimu itolewe kwa wahusika wanaojibu hoja ili kupunguza hoja zinazoletwa na CAG.
Waziri Kairuki pia amewataka kuhakikisha hoja hizo zinachambuliwa kwa kina ili kujua hoja zinazojibika na kuhitaji viambatanisho ili zifanyiwe kazi na kufutwa kabisa kwa wakati.
Vilevile, Waziri Kairuki ameagiza wasimamie ukusanyaji wa mapato na matumizi yake kwa kutumia mifumo ya ukusanyaji wa mapato na kuacha kutumia fedha mbichi.
Amewataka viongozi hao kuwa wanaangalia utaratibu wa kuwapata mawakala kwa kuangalia historia zao, uzoefu na ufanisi wao katika kazi ili kujirishisha kwa kuwa wanafanya kazi kwa niaba ya Halmashauri katika suala la ukusanyaji wa
mapato.
"Nendeni mkazihakiki na kuzikagua POS mashine ili kujua zinazofanya kazi, zilipotea na ambazo hazifanyi kazi ili kujiridhisha na kutolea taarifa kwa zile ambazo hazifanyi kazi
Ofisi ya Rais TAMISEMI," ameelekeza Waziri Kairuki.
Amesema Halmashauri zote nchini zinapaswa kuhakikisha wamejiunganisha na mfumo wa Tausi katika ukusanyaji wa mapato ifikapo Novemba, 2, mwaka 2022.
Amewataka kuhakikisha wanatumia mfumo wa utoaji mikopo ya asilimia 10 na kufanya ufuatiliaji wa urejeshwaji wa mikopo hiyo pia vikao vilivyowekwa kisheria vinafanyika kwa wakati kuanzia ngazi ya Kata hadi Mkoa.
Aidha, ameziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanajikita katika suala la usafi wa mazingira ili kupendezesha miji.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.